SERIKALI YAUNDA TIMU MAALUM KUMSIMAMIA MKANDARASI WA REA KILIMANJARO

Veronica Simba – Kilimanjaro

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameunda Timu maalumu inayojumuisha wataalamu mbalimbali wa Serikali ili kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro.

Ad

Alitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020 muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Chuo cha Ualimu Mong’are.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, muda mfupi baada ya kuwasha rasmi umeme katika Chuo cha Ualimu Mong’are, Agosti 17, 2020. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Sabaya.

Kuundwa kwa Timu hiyo itakayoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga kunatokana na kusuasua kwa Mkandarasi husika, Kampuni ya Urban & Rural Engineering Services Ltd katika kutekeleza kazi zake.

“Timu hii maalumu ya watu sita, itafanya kazi kwa muda wa siku 14 kuanzia  leo ili kuhakikisha Mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati, ifikapo Septemba 15 mwaka huu,” alifafanua Waziri.

Waziri alimwagiza Mkandarasi husika kuweka Magenge matano ya kazi katika Wilaya ya Hai ili kuharakisha kazi husika. Aidha, aliwataka Wakurugenzi wa Kampuni hiyo kuungana na Wafanyakazi wao ili kuongeza nguvu na msukumo wa kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Sabaya akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wilayani humo, Agosti 17, 2020.

Alikemea tabia ya Wakurugenzi hao kutokufika katika maeneo ya kazi na kuwaachia wafanyakazi wao pekee ambao hata hivyo Serikali imebaini hawalipwi mishahara yao kwa wakati hivyo kuchangia kuzorota kwa kazi.

Vilevile, alitoa maelekezo kwa Wakandarasi husika kutokuondoka Hai hadi watakapokamilisha kazi hiyo.

“Ninaagiza Wakandarasi hawa wakiwemo Wakurugenzi wao, wote wasiondoke hapa Hai hadi watakapokamilisha kazi. Aidha, ninaagiza wawe wanaripoti kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Hai, kila siku saa tatu asubuhi ili tujiridhishe kuwa wapo kazini. Mkuu wa Wilaya, tusaidie kusimamia hilo,” alisisitiza Waziri.

Maelekezo mengine aliyotoa Waziri ni kwa Wakandarasi kuhakikisha vibarua wote wanavaa nguo maalumu za kazi na kuwa na vifaa vyote vinavyowalinda na madhara zikiwemo kofia ngumu, buti na soksi za mikono.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) akimtambulisha Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga kwa wananchi wa Kitongoji cha Kambi ya Nyuki wilayani Hai, Agosti 17, 2020. Waziri alimteua Mhandisi Luoga kuongoza Timu maalumu itakayomsimamia Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini mkoani Kilimanjaro ili akamilishe kazi kwa wakati.

Aidha, alielekeza wafanyakazi na vibarua wote walipwe ujira wao kwa wakati huku akisisitiza kuwa Mkandarasi atakayebainika kutotekeleza maagizo hayo, atachukuliwa hatua kali za kisheria na kimkataba.

Awali, akitoa salamu za kumkaribisha Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Sabaya alipongeza utendaji kazi mzuri wa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo lakini akalalamikia utendaji unaosuasua wa Mkandarasi husika.

“Mkandarasi hajafanya kazi ya kutosha. Tulipaswa kuwa tumesimika transfoma 37 katika Wilaya yetu lakini hadi sasa amesimika transfoma saba tu.”

Waziri alimtaka Mkandarasi huyo kukamilisha kazi ifikapo Septemba 15, 2020 na akaahidi yeyé mwenyewe kwenda kuwasha rasmi umeme katika vijiji vyote vilivyosalia.

Timu iliyoundwa inajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO Makao Makuu na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Makao Makuu.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *