Imethibitishwa kuwa sasa Chuo cha Madini kilichokuwa chini ya Wizara ya Madini kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam.
Hayo yalithibitishwa Agosti 19, 2020 wakati wa Hafla ya Kukabidhi Chuo hicho Kampasi ya Dodoma na Nzega Kulelewa kwa muda na Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam katika hafla iliyofanyika katika Kampasi ya Nzega Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora .
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa Tukio Hilo ni moja ya hatua za uboreshaji wa Sekta ya Madini pamoja na kuhakikisha nchi ya Tanzania inazalisha wataalam wa kutosha na wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya madini kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Stashahada ili nchi iweze kusimamia rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia bila kutegemea wataalam kutoka nje.
Alisisitiza kuwa, Serikali inaamini kuwa, ulezi wa Chuo cha Madini kama ilivyoelezwa kwenye mchakato wa awali, kitaendelea kutoa mafunzo ya mchundo na mafundi sanifu katika sekta ya Madini lengo likiwa kukifanya kitengamae hatimaye kiweze kujiendesha.
Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Nzega
“Uleaji utakaotolewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ulenge kukiimarisha Chuo Cha Madini Kitaaluma, kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” Alisisitiza Nyongo.
Aliongeza kuwa, Mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na UDSM yasilenge kuondoa majukumu ya msingi ya Chuo Cha Madini.
“Ni matarajio ya Serikali na Wizara kuwa Chuo hiki kitafikia viwango vya Kitaaluma vinavyokubaliwa Kitaifa na Kimataifa,” alisema Nyongo.
Akielezea kwamba, kumekuwepo na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kutokuwepo kwa Sheria ya kuanzishwa Chuo Cha Madini; uvamizi wa maeneo hususan KampasiI ya Nzega na kuongeza kwamba anaamini changamoto hizo zitatuliwa chini ya ulezi huo na kwamba , hafla hiyo ni matokeo ya utatuzi wa changamoto hizo.
Pia, alizungumzia hatua mbalimbali ambazo zimechukukiwa na Serikali, ambazo zimepelekea Sekta ya Madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa, ambapo Mwaka 2019 iliongoza kwa Ukuaji kwa asilimia 17.7.
Alisema kutokana na jitihada hizi sasa mapato yanayotokana na madini yameongezeka ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 zilikusanywa Shilingi Bilioni 346 kutoka Shilingi Bilioni 194 Mwaka 2016/17, kwenye Mwaka 2019/2020 zlikusanywa zaidi ya Shilingi Bilioni 470 ambalo ndiyo lilikuwa lengo la Wizara.