MCHANGO WA SEKTA YA ELIMU NA MAFUNZO KATIKA MAPINDUZI YA KIUCHUMI

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Serikali imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Sekta ya elimu na mafunzo, kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa 2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025.

Ad

Serikali iliandaa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili kutoa mwelekeo wa elimu na mafunzo nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia na changamoto za elimu na mafunzo kitaifa, kikanda na kimataifa, ili kuongeza fursa, ufanisi na ubora wa elimu na mafunzo nchini na kufikia viwango vya rasilimaliwatu kwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Sera hii imeweka Dira ya elimu na mafunzo nchini kuwa ni “Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa” na Dhima yetu kuwa ni “kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu”.

Nyumba za walimu (sita katika moja) zilizopo katika shule ya Sekondari ya kutwa ya Sawe iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. (Picha na Daud Manongi – MAELEZO)

Akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma, Novemba 20, 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe magufuli pamoja na mambo mengine alisema, juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Aidha, Serikali itahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k.

Aliweka bayana kwamba Serikali itahakikisha kuanzia Januari 2016 elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure. “Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini” alisema Rais Magufuli.

Akizungumza mwezi Juni mwaka huu, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu (CWT), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwamoja ya vipaumbele vya Serikali yake ni kukuza na kuimarisha Sekta ya elimu nchini, na  kuwa Serikali itaiendeleza sekta hiyo hususan katika kupanua wigo na kuboresha elimu inayotolewa kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, sambamba na kuendelea kuajiri walimu .

Ni dhahiri shahiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza sera hiyo ya elimu nchini kwa kufanya mapinduzi yanayolenga kuzalisha wasomi na watendaji watakao iendeleza Tanzania ya viwanda na nchi yenye uchumi ulioimarika zaidi.

Mapinduzi hayo yanajidhihirisha katika maboresho ya sekta hiyo ambapo shule ya Sekondari ya kutwa iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imenufaika kupitia utekelezaji unaofanywa na Serikali wa kuboresha nyumba za walimu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu sita ndani ya moja (six in one) katika Shule ya Sekondari Sawe yenye jumla ya wanafunzi 213 unatajwa kuboresha mazingira ya kuishi walimu na kuongeza ufanisi wa kazi ya kufundishia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sawe, Gaudence Silayo anasema kuwa shule hiyo ilipoanza mwaka 2007 haikuwa na nyumba za walimu, badala yake walimu waliishi mitaani katika nyumba za kupanga na kutokana na hali ya hewa iliyopo katika eneo hilo ya mvua nyingi na matope walimu walipata shida na walifika shuleni kwa kuchelewa  jambo ambalo lilishusha kwa kiwango kikubwa ufaulu wa shule  hiyo.

“Mradi huu wa ujenzi wa nyumba sita katika moja ulipokuja kwa bajeti ya mwaka 2015/2016 wenye gharama ya shilingi 150,586,100 ambao ulikamilika mwaka 2017, basi kuanzia wakati huo walimu sita waliweza kuishi hapa shuleni, jambo hilo lilileta faraja na matumaini makubwa na liliongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa walimu” anasema Mwalimu Silayo

Aidha, akifafanua faida za kuwepo kwa nyumba hizo, mwalimu Silayo anasema kuwa shule iliandaa masomo ya ziada baada ya masomo ya darasani ambapo wanafunzi walifaulu vizuri, kidato cha pili walifaulu wote isipokuwa mwanafunzi mmoja na wanafunzi wa kidato cha nne walifaulu wote isipokuwa wanafunzi watatu.

Naye, mwalimu Germana Mtenga anayefundisha katika shule hiyo anasema kuwa faida ya kuwa na nyumba zinatoa fursa kwa walimu kutoa msaada wa masomo wa ziada kwa kwa wanafunzi hasa kwa sababu tayari walimu wamekuwa na utulivu, sambamba na kuwasaidia wanafunzi wa kike wanapokuwa wamepata matatizo mbalimbali.

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imejipambanua kuboresha sekta ya elimu nchini  kwa  kutoa elimu bila malipo katika shule za msingi na sekondari, tangu Disemba, 2015 hadi Februari, 2020 imetumia jumla ya shilingi Trilioni 1.01/=. Maboresho mengine ni pamoja na kuongezeka kwa  idadi ya shule za Msingi kutoka 16,899 zilizokuwepo mwaka 2015 hadi shule 17,804 mwaka 2020. Shule za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka 4,708 hadi 5,330 mwaka 2020.

 Fauku ya hayo, ukarabati wa shule kongwe za Sekondari 73 kati ya shule Kongwe 89, kujengwa mabweni 253 na nyumba za walimu na maabara 227, Serikali imetoa vifaa vya maabara vipatavyo 2,956 na kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi madawati  8,095,207 mwaka 2020.

Vilevile bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 341 kwa mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 450 mwaka 2019/2020.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *