Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja,amekagua ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha Umeme wa Megawati 2115 kwa kutumia Maporomoko ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji wa Julius Nyerere( JNHPP).
Mhandisi Masanja amefanya ukaguzi huo hususani katika eneo la Bwawa la Maji ili kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi, Agosti 22, 2020.
Ad
Mhandisi Masanja alitembelea maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi huo likiwemo Handaki la kuchepusha Maji ya Mto, Handaki la kupeleka Maji katika mitambo ya kufua Umeme, pamoja sehemu itakapojengwa jengo maalum la kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme(Controlroom).
Vilevile alikagua mitambo ya kusaga na kuchakata kokoto, pia na mitambo ya kuchanganya Zege ambayo inatumika katika shughuli za ujenzi katika eneo la mradi ikiwemo bwawa husika.
Ikumbukwe kwamba Kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza rasmi mwezi Juni 15, 2019 ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 36, na unatarajiwa kukamilika mwezi June 2022, chini ya Mkandarasi wa ubia wa Kampuni Arab contractors na Kampuni El Sewedy.
Mradi wa JNHPP umeiwezesha na kuitambulisha Tanzania kuingia katika ulingo wa Kidunia na kushika nafasi ya 70 kwa kujenga Bwawa kubwa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji kati ya mabwawa yote ya aina hiyo duniani.
Vilevile umeiwezesha kushika nafasi ya nne kwa nchi za Afrika ambapo la kwanza ni Renaissance lililopo Ethiopia linalozalisha (Megawati 6450), la pili ni Mambila nchini Nigeria (Megawati 3050), la tatu ni Kakula Kabako nchini Angola (Megawati 2170.
Na katika Ukanda wa Afrika Mashariki linashika nafasi ya kwanza,likifuatiwa na Kaborabasa la Msumbiji linalozalisha megawati 1,245, Kafue Gorge nchini Zambia litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1,145 pindi litakapokamilika mwaka 2024, na Karuma nchini Uganda linalozalisha megawati 600.
Na Zuena Msuya, Morogoro
N.B: Tafadhali soma Jarida la Wizara ya Nishati, linalotoka kila mwisho wa mwezi ili kupata habari motomoto kwa kina zaidi zinazohusu sekta ya Nishati na Taasisi zilizochini yake, pia linapatikana katika tovuti ya wizara ambayo ni www.nishati.go.tz.