Na Zuena Msuya, Morogoro
Timu ya Kitaifa ya Wataalamu inayofuatilia hali ya uhifadhi wa rasilimali ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, imesema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Julius Nyerere( JNHPP)uzuia Gesi Joto ya takribani Tani Milioni 7.6 katika uso wa dunia( Ozone layer) kwa mwaka mzima Duniani.
Wataalamu hao walieleza hayo baada ya kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa JNHPP wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo iliyofanyika Septemba 19, 2020, mkoani Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mkuu wa Idara ya Mazingira kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Richard Muyungi, alisema kuwa uwepo wa mradi huo kutaisaidia dunia kupambana na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi ambao umekuwa ukisababishwa na vyanzo mbalimbali.
Dkt. Muyungi alisema uso wadunia umekuwa ukichafulia kutokana vya vyanzo mbalimbali baadhi yako ni uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia Joto Ardhi pamoja na Gesi.
“Mradi huu unafaida za ziada tofauti na zile zinazoelezwa, tumefanya utafiti tumebaini kuwa endapo mradi huu usingejengwa basi tungezalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingine kama gesi na Joto ardhi ambazo zingezalisha Gesi Joto takribani milioni 7.6 kwa mwaka, ambazo zingechafua mazingira na uso wa dunia, lakini kwa kutumia maji hatutazalisha gesi hizo”,alisisitiza Dkt. Muyungi.
“Kiukweli mradi huu ndiyo mradi pekee Afrika, ambao unaweza kuzuia uzalishaji wa gesi hii na hivyo kuionyesha dunia pamoja na Jumuia za Kimataifa kuwa licha ya faida zote zinazoelezwa, mradi huu unafaida za ziada ambayo tunaisadia dunia kupambana na madiliko ya tabia nchi pamoja na uchafuzi wa mazingira licha ya kuwa gesi joto zinazosababisha hali hiyo hazizalishwi kutokana na vyanzo vyetu vya nishati ”, alisema Dkt.Muyungi.
Aliendelea kusema kuwa, ukiwa na maji ya uhakika ya takribani Kilomita Mia (100) hadi Ishirini na tano(25), eneo hilo litakuwa na vyanzo muhimu vya maji, yatakayotumiwa na wanyama na kustahimili katika eneo hilo kwa muda mrefu, tofauti ilivyokuwa hapo awali kabla ya kuwa na bwawa hilo, wanyama hao wasingeweza kustahimili na kuyatumia muda wote na wakati mwingine wanahama eneo husika ama kwenda umbali mrefu kutafuta maji.
Dkt. Muyungi aliongeza kuwa baada ya eneo hilo kutangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa, kumeongeza ulinzi wa wanyama, mimea pamoja na uasilia wake ambapo endapo usingefanywa mradi huo na kuwa eneo na hifadhi ya taifa,viumbe wa eneo hilo wangedhulumiwa na eneo hilo kupoteza ualisia wake kwa sababu ya ulinzi kuwa hafifu pamoja na shughuli mbalimbali za kibinadamu tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa JNHPP kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Yusuph Msembele, alisema kuwa lengo ziara hiyo ni kuwaonyesha wataalamu wa timu hiyo maendeleo ya mradi ili wapate hamasa katika kusimamia matumizi bora ya rasilimali maji katika Bonde la Mto Rufiji kwa kuwa taasisi zao ndizo zenye dhamana ya kutekeleza usimamizi wa sheria za uhifadhi.
Hivyo Mhandisi Msembele,aliwashauri na kuwasisitiza wajumbe wa Timu hiyo kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha wananchi kuzingatia matumizi bora na sahihi ya maji katika ukanda wa vyanzo vya maji ya Bonde la Mto Rufiji.
Naye Mhandisi mkazi na Mshauri wa mradi huo, Mhandisi Mushubila Kamuhabwa, aliieleza timu hiyo kuwa, ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na uko katika hatua nzuri za utekelezaji wake.
Timu hiyo ya wataalamu inaundwa na Wajumbe Kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI),Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira,Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera na Uratibu, Wizara ya Nishati, na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji,Wizara ya Maliasili,Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira, (NEMC), Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) na Bonde la Mto Rufiji.