WATU 18 WAKUTWA NA SHINIKIZO LA DAMU, ZAIDI YA ASILIMIA 50 WANA UZITO ULIOPITILIZA, JUKWAA LA ONE STOP JAWABU – MBAGALA

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zenais Ngowi akitoa maelekezo ya jinsi ya kujaza fomu ya uelewa wa magonjwa ya moyo kwa mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo katika viwanja vya Mbagala Zakheem wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo Taasisi hiyo ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imewaibua watu 21 wenye matatizo mbalimbali ya moyo, 18 wamekutwa na shinikizo la damu, walipochunguzwa afya zao katika Viwanja vya Mbagala Zakheem  wilayani Temeke kwenye jukwaa la One Stop Jawabu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu alisema watu 16 kati ya 18 waliokutwa na shinikizo la damu walikuwa hawajitambui kwamba wanakabiliwa na tatizo hilo.

Ad
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Steven Lugu akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika viwanja vya Mbagala Zakheem wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo wananchi 103 walifika katika banda hilo na kupewa huduma za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo.

“Hii ni sawa na asilimia 18, yupo mmoja ambaye tumemkuta ana shinikizo la damu 200 chini ya 110, ni mara yake ya kwanza amekuja kufanyiwa uchunguzi, ni shinikizo ambalo lipo juu mno, tulidhani labda amepata mshtuko alipofika hapa.

“Tulimtaka akae kidogo apumzike, tukamfanyia tena uchunguzi na kukuta hali ikiwa vile vile, endapo tusingemgundua alikuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha, tumempa rufaa kuja JKCI kwa matibabu,” amebainisha.

Wananchi waliofika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika viwanja vya Mbagala Zakheem wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu wakipata huduma mbalimbali za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo ambapo watu 103 walifika katika banda hilo na kupewa bila malipo huduma za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo.

Dk. Rweyemamu amesema mtu mmoja kati ya hao walifanyiwa uchunguzi amekutwa na tatizo la kuziba kwa mshipa wa damu kwenye moyo, watu 10 wamekutwa na kisukari.

“Watu 50 tuliwachunguza afya ya moyo kwa kutumia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na 53 tuliwafanyia kipimo cha kuangalia umeme wa moyo (Electrocardiography –  ECG)  wawili kati ya hao tuliowachunguza tulikuta ‘valve’ zao za moyo zina tatizo,” amebainisha.

Ameongeza “Asilimia 50 ya watu wote tuliowachunguza wana uzito uliopitiliza, hii ni hatari kwa afya ya mioyo yao. Watu 21 tumewapa rufaa kuja kwenye Taasisi yetu kupitia Hospitali yao ya Mbagala Zakheem ili tuwafanyie uchunguzi zaidi na kuwapa matibabu.

Amesema ndani ya banda lao pamoja na uchunguzi wa afya ya moyo, vile vile walitoa elimu ya lishe kwa wananchi hao ili waweze kulinda afya yao ya moyo na mwili kwa ujumla.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zenais Ngowi akitoa maelekezo ya jinsi ya kujaza fomu ya uelewa wa magonjwa ya moyo kwa mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo katika viwanja vya Mbagala Zakheem wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo Taasisi hiyo ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo.

“Tumewaelimisha wazingatie ulaji unaofaa, waepuke vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari nyingi na uvutaji wa sigara, ili kuepuka magonjwa yasiyo ambukiza ikiwamo haya ya moyo.

“Tumewashauri pia kukata bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata matibabu maana gharama ni kubwa endapo ukiwa huna bima ya afya ni changamoto,” amesema.

Wakizungumza mara baada ya kupatiwa huduma katika banda la Taasisi hiyo wakazi wa Mbagala  ameipongeza Serikali na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe kwa kupeleka jukwaa hilo katika eneo hilo kwani wameweza kufikiwa na kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo na hatimaye wengine wamelutwa na matatizo na kupewa huduma ya matibabu.

“Kupitia vyombo vya habari nilisikia siku ya leo wataalamu wa moyo watakuwepo mahali hapa nikaamua kuja kupima afya yangu. Nimeweza kupima na kufahamu hali yangu ikoje. Ninashukuru sana kwa huduma niliyoipata”,.

“Ninawashauri wananchi wenzangu wanaposikia wataalamu kama hawa wanafanya upimaji wajitokeze kwa wingi kupima afya zao kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kufahamu wanakabiliwa na matatizo gani ili waweze kupata matibabu kwa wakati  na kama hawana matatizo wataweza kujikinga”, alisema Hamza Juma mkazi wa Chamazi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *