Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) imeandaa Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA, “Tanzania Annual ICT Conference 2020” ambalo limepangwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 OKtoba, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Taarifa rasmi imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula, alipozungumza na waandishi wa habari, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Dkt. Chaula amesema kuwa, Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo atakuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Aloyce Kamwelwe ambapo atazindua rasmi Usajili wa wataalamu wa TEHAMA nchini kwa kutoa vyeti vya usajili kwa wataalam 100 wabobezi wa TEHAMA nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 inayotaka kuwa na nguvukazi yenye uwezo na maadili ili kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na mchango wake katika maendeleo ya nchi,
“Kwa muda mrefu tumekuwa na wataalamu wanaosimamia miundombinu na mifumo muhimu ya TEHAMA pasipo kutambuliwa uwezo na maadili yao, hivyo siku hiyo Waziri mwenye dhamana ya TEHAMA atatoa vyeti kwa wataalamu 100 wa kwanza ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi usajili wa wataalamu wa TEHAMA , kuwatambua na kuwaendeleza ili kuongeza ufanisi na utendaji, ambapo kupitia TEHAMA uzalishaji viwandani utaongezeka na nchi kuingia katika kizazi cha nne cha mapinduzi ya viwanda”, alizungumza Dkt. Chaula
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FCDT) Sosthenes Kewe, amesema kuwa Mfuko umefadhili Kongamano hilo ili kuunga mkono azma ya Serikali ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali, ambapo kufanikisha hili ni kupitia ubunifu na matumizi mtambuka ya TEHAMA kwa Sekta zote za kijamii na kiuchumi zikiwemo Sekta za fedha katika kuchochea mabadiliko hayo ili nchi kupata mafanikio mtambuka.
Na Faraja Mpina, WUUM, Dodoma
Ameongeza kuwa, Serikali imejenga miundombinu ya mawasiliano, mifumo, sheria, taratibu na miongozo mbalimbali ya mawasiliano hivyo tayari msingi wa kuelekea katika uchumi wa kidijitali umeshawekwa, kinachotakiwa kufanyika sasa ni kufikia na kuwezesha matumizi ya TEHAMA kwa watendaji wa Serikali, watoa huduma na wananchi kwa ujumla, ili kwa pamoja tuipeleke nchi kwenye uchumi wa kidigitali.
Kongamano la TEHAMA linaratibiwa na Tume ya Taifa ya TEHAMA, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Samsoni Mwela amesema kongamano hilo litakuwa na mijadala mbalimbali kuhusu dira,fursa, ujuzi, ubunifu, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye uchumi endelevu wa kidijitali kwa kutumia wataalamu wabobezi wenye uwezo wa kutengeneza mifumo yetu wenyewe na kuisimamia.
Mwela ametilia mkazo kuhusu wataalamu 100 wataopewa vyeti vya usajili kuwa ni wataalamu waliobobea katika miundombinu, masafa, kutengeneza mifumo, usalama wa mitandao na katika maeneo mengine muhimu na wezeshi katika kufanikisha na kuendeleza matumizi ya TEHAMA na mabadiliko ya kuelekea uchumi wa dijitali.