Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha programu maalum ya kuwatambua, kuwasajili na kuwaendeleza wataalamu, wabunifu na wabobezi katika nyanja ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwatumia katika kukuza uchumi wa nchi ambao kiuhalisia unaendeshwa na teknolojia hiyo muhimu.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa, kuna wahitimu wengi wenye uwezo mkubwa kiutendaji, wabunifu na wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA, ni muda muafaka kwa Serikali kuwatambua walipo na wanachokifanya ili kuwatumia vyema kwa maendeleo yenye tija kwa nchi.
Waziri Kamwelwe amesema kuwa, Serikali imeanza kwa kutoa vyeti vya usajili kwa wataalamu 100 wa kwanza wa TEHAMA huku mchakato wa kupitisha Sheria rasmi Bungeni ukiwa katika hatua nzuri.
“Baada ya uchaguzi Bunge litapelekewa Sheria ili ipitishwe na kuwa rasmi ambapo itasaidia kuwatambua na kuwasajili wataalamu wa TEHAMA kwa mujibu wa sheria kupitia Tume ya Taifa ya TEHAMA ambapo itasaidia Serikali kutumia nguvukazi muhimu katika nchi ambayo miaka ya nyuma ilitumika na nchi nyingine kutengeneza mifumo ambayo baadae nchi inakuja kuuziwa kwa mabilioni ya fedha,” alisema Kamwelwe
Na Faraja Mpina -WUUM Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt Zainabu Chaula amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni Sekta mtambuka, wezeshi ya kimkakati na kiuchumi na imefanya kazi kubwa katika kuutandaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwahakikishia wananchi mawasiliano ya uhakika.
Kongamano hili linawaweka pamoja wataalamu wa TEHAMA ili kujadili kwa kina maeneo mbalimbali ya kimkakati kuhusu matumizi ya TEHAMA, ili hata wale wasiofahamu vizuri nini Serikali imefanya na imewekeza vipi katika TEHAMA waweze kufahamu na kuitumia vema kwa maendeleo ya nchi yetu, alizungumza Dkt Chaula
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Samson Mwela, amesema kuwa Kongamano la TEHAMA la Mwaka huu linafanyika kwa siku 3, Oktoba 7, 8 na 9 likiwa ni Kongamano la Nne toka makongamano hayo yaanze kufanyika, lenye kaulimbiu inayosema, “ Kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda”, ambapo maeneo yanayoangaliwa ni kuhusu dira, ujuzi na ubunifu kuelekea uchumi wa viwanda.
“Ili kuelekea katika uchumi wa viwanda ni lazima kuwe na wataalamu wazalendo wa TEHAMA wa kutosha ambao watatumika katika kuipeleka nchi katika Mapinduzi ya uchumi wa viwanda kidijitali”, alizungumza Mwela