Mkoa wa Kagera umekamilisha jumla ya miradi ya maji 73 yenye thamani ya shilingi 62,516,688,102 hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kutoka asilimia 42 iliyokuwepo mwaka 2015 katika miji hadi kufika asilimia 65 iliyopo sasa na kwa vijijini kutoka asilimia 53 hadi asilimia 67.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), mkoa wa Kagera Mhandisi Warioba Sanya amesema hayo na kuongeza lengo ni kufika zaidi ya asilimia 85 kwa vijijini.
Amesema kwa miji ongezeko hilo ni kwa miji ya wilaya na mkoa ambapo inatarajiwa kiwango cha upatikanaji maji kuongezeka kwa sababu ya uwekezaji katika miradi inayoendelea, akitolea mfano wa Manispaa ya Bukoba ambapo kwa sasa upatikanaji maji ni asilimia 90 ambayo itapanda hadi kufikia asilimia 95 ifikapo Juni 2021 baada ya mtandao wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kuongezwa katika maeneo ya pembezoni.
Amefafanua kuwa kuna ujenzi wa miradi mikubwa ya maji mjini inayohusisha ujenzi wa miradi ya Maji katika mji wa Kayango wilayani Karagwe, Mji wa Kyaka-Bunazi wilayani Misenyi, Mjini Kemondo hadi Maruku wilayani Bukoba, Mji wa Biharamulo na ujenzi wa mradi wa mifumo ya maji taka Mjini Bukoba
Mhandisi Warioba amesema thamani ya miradi ya maji ambayo imekamilika na ambayo inatekelezwa sasa, ni kiasi cha shilingi 216,568,311,607.
Mkoa wa Kagera unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 3,127,608 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012