Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Oktoba, 2020 ametembelea Msikiti Mkuu uliojengwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam kwa ufadhili wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco.
Msikitini hapo, Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zuberi Ally, Balozi wa Morocco hapa nchini Mhe. Abdelilah Benryane na viongozi wengine wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ngazi ya Taifa na Mkoa wa Dar es Salaam.
Ad
Ujenzi wa Msikiti huo ulioanza mwaka 2019 baada ya Mhe. Rais Magufuli kumuomba Mfalme Mohammed VI (aliyekuwa katika ziara ya Kitaifa hapa nchini) ajenge Msikiti mkubwa kwa ajili ya Waislamu wa Tanzania, umekamilika kwa asilimia 100 na hivi sasa unasubiri kuzinduliwa rasmi.
Baada ya kuutembelea na kujionea ukiwa umekamilika, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na ubora wa hali ya juu wa Msikiti huo, jinsi unavyovutia na amesema ameridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuandika barua ya kumualika Mfalme Mohammed VI kuja hapa nchini kuzindua Msikiti huo kama alivyoahidi na amemuomba Balozi wa Morocco hapa nchini Mhe. Benryane kutanguliza salamu zake za shukrani kufuatia kukamilika kwa ujenzi huo.
Wakiwa Msikitini hapo, Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zuberi Ally ameomba dua kwa ajili ya Taifa, amemuombea Mhe. Rais Magufuli, na pia shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo.