Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amewataka watumishi wa Wizara yake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mapato na matumizi ya fedha za umma ili kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyotolewa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, akizindua Bunge la 12.
Hayo aliyasema wakati akipokelewa katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma baada ya kuteuliwa na kuapichwa na Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kushika wadhifa wa Waziri wa Fedha na Mipango kwa mara ya pili, Ikulu ya Chamwino, Jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema kuwa bado kuna shida kubwa katika eneo la matumizi ya fedha za umma, kwa kuwa fedha zinazopelekwa kutekeleza miradi mbalimbali hazitumiwi vizuri na kusababisha miradi mingine kutekelezwa chini ya kiwango.
“Tunahitaji jicho la pekee katika Halmashauri za Wilaya na Miji, tunapeleka fedha za miradi lakini mimi nakadiria kuna upotevu wa takribani asilimia arobani ya fedha hizo kwahiyo ni lazima tuwe na jicho kali ili kuokoa fedha za wananchi”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema mpango wa kununua Ndege, Meli na vitu vingine katika kipindi cha miaka mitano itafanikiwa iwapo kila mmoja katika nafasi yake atasimama imara kuhakikisha mapato yanakusanywa na yanatumika kikamilifu.
Alisema kuwa Watanzania wanamatarajio makubwa kutoka katika Serikali yao hivyo watumishi wa Wizara ambao ni kama kitovu cha maendeleo wanatakiwa kuhakikisha matarajio hayo yanafikiwa.
Dkt. Mpango amewashukuru Watumishi wa Wizara yake kwa utendaji kazi mzuri kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini ameomba waongeze jitihada na maarifa katika kutekeleza miongozo mbalimbali ikiwemo Hotuba ya Rais ya kufungua Bunge la 12, Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuweka mikakati Madhubuti ya kufanikisha utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, alimhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwamba Menejimenti imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa inaendelea kutoa ushauri wa kitaalam ili nchi iweze kufikia malengo iliyojiwekea katika kukuza uchumi.