Serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kujidhatiti katika kuboresha utoaji huduma za Afya kwa wananchi ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, uboreshaji wa huduma za chanjo, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe wakati akifungua Mkutano wa 21 wa kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya ulioandaliwa kwa pamoja na Wizara yake na Ofisi ya Rais TAMISEMI ukishirikisha Wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya nchini unaoendelea Jijini Dodoma.
Prof. Mchembe amesema kuwa, kikao hicho kina umuhimu mkubwa sana katika Wizara na Sekta ya Afya kwa ujumla kwa sababu ndio kinachoweza kuweka mikakati ya nini kifanyike miaka mitano ijayo, baada ya kupitia mikakati ya miaka mitano iliyopita na kuona mafanikio na changamoto zake.
“Kama Serikali tumefanikiwa kuboresha katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, huduma za chanjo, vifaa na vifaa tiba pamoja na uboreshaji wa utoaji huduma zinazotolewa na Watumishi wa Afya” amesema Prof. Mchembe.
Aidha, Prof. Mchembe amesema mpango mkakati wa tano unaoenda kuanza ni matokeo ya ule wa nne ambapo unaangazia mafanikio, na kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha Sekta ya Afya.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, kama wasimamiaji wa utekelezaji wa Sera katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za mitaa wapo tayari kutekeleza maagizo na miongozo itayotolewa kupitia kikao hicho cha tathmini ya Sera kilichohudhuriwa na Wadau wote wa Sekta ya Afya nchini.
Na, Rayson Mwaisemba WAMJW- DOM
“Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameeleza mambo mengi, sisi tupo kama Wadau ambao tunasimamia utekelezaji kwenye ngazi ya Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa tunasubiri maelekezo na miongozo ya Kisera ili kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo tuweze kutekeleza kwa kasi ile ile” alisema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga amesema kuwa, kikao hicho cha Sera hupokea mambo yote katika Sekta ya Afya yaliyofanyiwa tathmini na yaliyokubalika kuwa ndio yatakuwa malengo na muelekeo wa Sekta ya Afya nchini.