Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula amewataka watumishi wa Sekta hiyo kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa pamoja katika kubaini na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa malengo ya Sekta.
Dkt. Chaula amezungumza hayo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku tano kwa wataalamu wa Sekta hiyo ya kuandaa Rejista ya Vihatarishi (Risk register) uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo, jijini Dodoma.
“Tunatakiwa kuhakikisha malengo ya Sekta yanatekelezeka kwa kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kusababisha malengo hayo yasitimie, ikiwa ni pamoja na kupeleka mawasiliano ya uhakika nchi nzima”, alizungumza Dkt. Chaula
Aliongeza kuwa Sekta hiyo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia na kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo watendaji wanatakiwa kujipanga kuhakikisha miundombinu hiyo ipo salama dhidi ya uharibifu na kuhakikisha Serikali haipati hasara.
Aidha, Dkt. Chaula amewasisitiza watendaji wa Sekta hiyo wasikariri takwimu, wahakikishe takwimu zinaboreshwa mara kwa mara ili kupata takwimu halisi ambazo zitasaidia kupima utendaji wa Sekta na kujiridhisha malengo yamefikiwa kwa asilimia ngapi.
Na Faraja Mpina – WUUM
Naye, Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt Ernest Mwasalwiba kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, ameipongeza Sekta ya Mawasiliano kwa hatua hii ya kuandaa rejista ya vihatarishi kwasababu ni hatua muhimu sana kwa taasisi ya umma kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea.
Aliongeza kuwa, kuandaa rejista ya vihatarishi ni hatua ya mwanzo kabisa na haitakuwa na maana kama vihatarishi hivyo havitafanyiwa kazi ya kuvidhibiti visitokee ili Sekta kutimiza malengo yake.
Kwa upande wa mratibu wa mafunzo hayo, CPA, Joyce Christopher, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Sekta hiyo amesema kuwa uandaaji wa rejista hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mfumo wa kusimamia vihatarishi vya Sekta ya Mawasiliano ili kuendana na matakwa ya Serikali katika kuhakikisha kuwa kila taasisi ya umma inakuwa na nyaraka hizo za kubaini na kudhibiti vihatarishi ili taasisi hizo ziweze kufikia malengo zilizojiwekea.