Kwa mara ya kwanza bandari ya Tanga imeandika historia baada ya meli kubwa ya Mv Star Eos yenye urefu wa mita 200 kutia nanga karibu kabisa na gati la bandari ya Tanga baada ya bandari hiyo kufanyiwa maboresho ikiwemo kuongezwa kina cha maji.
Meli hiyo iliyobeba shehena ya “Clinker” Tani 55,000 zinazo pelekwa nchi ya Jirani ya Rwanda ni mara yake ya kwanza kutia nanga katika bandari ya Tanga na kuandika historia hiyo.
Akizungumza wakati wa kupokea meli hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella amemshukuru Mhe Dkt.John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Tanzania kwa maamuzi yake ya msingi ya kuelekeza TPA kuanza kuchimba bandari ya Tanga wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi wa bomba la mafuta Chongoleani.
Ameongeza kwa kusema kuwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Nchi kwa sasa hakuna sababu tena ya kushusha shehena katika bandari za Nchi jirani kwani bandari ya Tanga kwa sasa imeboreshwa na meli yoyote inaweza kutia nanga.
Kwa upande wake Kaimu Meneja bandari ya Tanga Bw Donald Ngaire amesema kuwa baada ya bandari ya Tanga kufanikiwa kusogeza meli mpaka mita 200 kutoka gatini kutapunguza gharama za uendeshaji ambapo awali meli zilikuwa zinatia nanga umbali wa km 1.7 kutoka bandarini hivyo gharama za uendeshaji zilikuwa ni kubwa sana.
Naye mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mh Ummy Mwalimu ameongeza kwa kusema kuwa kufanya vizuri kwa bandari ya Tanga ni kufanya vizuri kwa uchumi wa watu wa Tanga ambapo ni mojawapo ya ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni na kusisitiza zaidi kwa kusema kuwa maboresho ya bandari ya Tanga yatasadia vijana wengi hasa wakazi wa Tanga kupata ajira katika bandari hiyo.