DKT. MPANGO AAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO LA TANGAWIZI KIGOMA

Na Josephine Majura, Kigoma

Waziri wa Fedha na Mipango,  Dkt. Philip Isdor Mpango, ameahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la soko la zao la biashara la Tangawizi linalolimwa kwa wingi Kata ya Munzeze wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Dkt. Mpango ametoa ahadi hiyo katika Kata ya Munzeze mkoani Kigoma, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo ambapo amesema atatafuta masoko ndani na nje ya nchi ili wananchi wa mkoa wa Kigoma waweze kufaidika na kilimo cha zao hilo la biashara linalotegemewa na wananchi wengi kujipatia kipato.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akikaribishwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, kuzungumza na Wananchi wa Munzeze alipotembelea Kata ya hiyo iliyopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

“Nikiwa kwenye kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu nilishuhudia wafanyabiashara kutoka nchini Burundi wakinunua Tangawizi mbichi kwa bei ya chini na kuipelekea Tangawizi hiyo nchini mwao na kuichakata kisha kutuletea hapa nchini na kutuuzia kwa bei ya juu, hili halikubaliki, sisi tunatakiwa kuongeza thamani ya Tangawizi na kuiuza nchini mwao” alisema Dkt. Mpango

Sambamba na hilo Dkt. Mpango, aliwaahidi wananchi wa Kata ya Munzeze kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule ya Sekondari Kigogwe inayojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuboresha elimu katika Kata hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, alisema kuwa Wilaya yake inakabiliwa na lindi la umasikini kwa wananchi wake na kumwomba Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, Mhe. Dkt. Philip Mpango, kuwasaidia wananchi wa Wilaya hiyo kuondokana na hali hiyo kwa kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo zao la Tangawizi

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Wananchi wa Kata ya Munzeze, ambapo ameahidi kutafuta namna bora ya kuhakikisha zao la Tangawizi linaongezewa thamani na kutafutiwa soko la uhakika ili kuinua uchumi wa wananchi wa Kata hiyo, mkoani Kigoma.

Alieleza kuwa changamoto ya bei ya zao la Tangawizi inamsononesha kwani wananchi hususani wa Kata ya Muzeze ambao ni wakulima wazuri wa Tangawizi wanauza kilo moja ya zao hilo kwa kati ya shilingi 400 hadi shilingi 700, bei ambayo ni ndogo na haiwanufaishi wakulima.

“Nimeingia kwenye mitandao kutafuta mashine za kuongeza thamani ya zao la Tangawizi ambapo nimeona kuna mashine za kuosha Tangawizi, kuchambua, kuchakata na kufungasha zao hilo na zana hizi zikipatikana kwa wananchi wa Munzeze wataondokana na changamoto hiyo ya kuuza Tangawizi ghafi kwa bei ya hasara” Alisema Kanali Ngayalina

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akicheza ngoma na vikundi vya Upendo na Mkombozi, alipotembelea Wilaya ya Buhigwe, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kishindo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na yeye binafsi wakati wa uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Naye Diwani wa Kata ya Munzeze Mhe. Wilson Vyabhoze, amemuomba Waziri wa Fedha na Mipango, kuona namna ya kuanzisha Taasisi ambazo zitakuwa zinauza mbegu za mazao mbalimbali likiwemo Tangawizi ili kuwarahisishia Wananchi upatikanaji wake kwa kuwa ardhi yao ina rutuba ya kutosha.

Mkazi wa Kata ya Munzeze Bw. Yohane  Peter  amemuomba Dkt. Mpango kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifungashio vya kisasa vya Tangawizi ili zisiharibike haraka.

Katika ziara hiyo Dkt. Mpango ametembelea Kata ya Janda, ambapo Wananchi wa eneo hilo waliomba atatue changamoto ya Zahanati na kuahidi kushughulikia kwa haraka jambo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani) njia ya kuwasaidia wananchi wa Kata ya Muzeze, Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, kuondokana na umasikini kwa kuongeza thamani ya zao la Tangawizi linalolimwa kwa wingi na wananchi hao.

Vile vile Waziri Mpango, alitembelea Kata ya Bukuba ambapo aliahidi kumalizia ujenzi wa Zahanati mbili ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi hadi hatua ya renta kwa ajili ya kuhudumia Kijiji cha Bukuba na Kijiji cha Kibuye mkoani Kigoma.

Aidha aliongeza kuwa Serikali itajenga maabara katika Shule ya Sekondari ya Bwafuu ili kuboresha mazingira ya shule hiyo ili kutoa Wanafunzi wenye uelewa wa nadharia na vitendo katika masomo ya sayansi.

Dkt. Mpango aliwasisitiza Wananchi wa Munzeze kuendelea kudumisha amani na usalama wa nchi kwa kuwa ndiyo kitu muhimu katika maendeleo yoyote yale kwa kuwa Mkoa huo upo mpakani na nchi jirani ya Burundi

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiteta jambo na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Munzeze Bw. Msaki Emmanuel alipotembelea kituo hicho kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

“Amani ni kitu muhimu sana kwenye maisha yetu ya kila siku, bila amani biashara haziwezi kufanyika, bila amani Watoto hawataweza kwenda shule, bila amani shughuli za kimaendeleo hazitaweza kufanyika, ndugu zangu tuendelee kuidumisha amani yetu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu”. Alisisitiza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi na kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la Buhigwe  kwa kumchagua kwa kura za kishindo, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeye binafsi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Katika ziara hiyo amepanga kutembelea Kata nane kati ya ishirini zilizopo kwenye Jimbo lake la Buhigwe mkoani Kigoma, hadi sasa ameshatembelea Kata tano ikiwemo Munanila, Mwayaya, Munzeze, Janda na Bukuba.

Unaweza kuangalia pia

DKT MABULA AHIMIZA KASI YA UPIMAJI ARDHI BAHI

Na Munir Shemweta, BAHINaibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.