Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili nyingi zinazoweza kuifanya nchi hii kuondokana kabisa na umasikini na utegemezi, hivyo kujiendesha bila kutegemea misaada toka nje ya nchi.
Licha ya kuwa na hifadhi za taifa za wanyama, bahari, maziwa, mito na milima na mabonde, nchi hii imejaliwa pia kuwa na madini, bidhaa muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Takriban madini aina zote yanayopatikana duniani yapo Tanzania ikiwemo Tanzanite inayopatikana nchini pekee. Huu ni utajiri kwa vizazi na vizazi endapo Yyataendelea kudhibitiwa, kusimamiwa,kulindwa na kutumiwa ipasavyo. Yataliingizia Taifa mabilioni ya shilingi.
Juhudi za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kutumia vizuri rasilimali ya madini zimeifanya Tanzania kuingiza mabilioni ya fedha ambazo zinatumika katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya Afya, Elimu na Miondombinu ya barabara, reli na umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ambaye ni muasisi wa mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini, Dkt. John Pombe Magufuli anasema haya kuhusiana na madini: “Kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini. Mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019.”
Aliongeza kwa kusema, “Zaidi ya hapo, kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7. Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge la 11 kwa kutoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa mafanikio haya.”
Fedha iliyopatikana kutokana na madini yaani bilioni 527 inaweza kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka na nusu, inaweza kujenga vituo vya afya 1,150 au inaweza kulipia gharama ya elimu ya awali hadi sekondari kwa kipindi cha miaka miwili (yaani miezi 24).
Sekta ya Madini ikiendelea kusimamiwa vyema maendeleo makubwa katika nchi yatapatikana na kuibadilisha Tanzania kiuchumi na kuingia uchumi wa kati wa juu hadi kufikia uchumi wa juu wa nchi zilizoendelea kama vile Marekani, Uingereza, Sweden Ujerumani, China na nyinginezo ndani ya kipindi kifupi.
Akionyesha dhamira yake ya dhati kuhusu mchango wa madini katika kukuza uchumi wa Taifa, Rais Magufuli aliongeza, “Kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa madini yetu, (kama tulivyofanya kwa kujenga Ukuta Mirerani) kwa kuimarisha Sheria zetu ili madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato. Aidha, tunakusudia kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kwa kuzingatia mfano wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick yaliyowezesha kuundwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Corporation.”
Ujenzi wa ukuta wa Mirerani umedhibiti kwa kiwango kikubwa utoroshwaji wa Tanzanite na kufanya nchi hii kupata mauzo makubwa ya madini hayo. Zaidi ya hayo amepatikana bilionea mzawa kutokana na udhibiti huo Bwana Saniniu Laizer ambaye amejipatia zaidi ya shilingi bilioni11kwa kuiuzia Serikali ya Tanzania madini ya Tanzanite.
Aliyekuwa Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema,“Ujenzi wa ukuta kuzunguka machimbo ya madini eneo la Mirerani na kuweka vifaa vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa madini yaTanzanite ambayo ni rasilimali ipatikanayo Tanzania pekee inalindwa. Kufuatia uwekezaji huo, sote tumeshuhudia kuongezeka mara dufu kwa mapato yatokanayo na madini ya Tanzaite katika eneo hilo hususan kutoka kwa wachimbaji wadogo kutoka shilingi 166,094,043 kabla ya kujenga ukuta hadi shilingi 2,150,000,000 baada ya kujengwa kwa ukuta.”
Lilikuwa jambo la kushangaza kuona Tanzania haikuwa ya kwanza wala ya pili hata ya tatu kwa kuuza Tanzanite duniani wakati madini hayo yanapatikana Tanzania pekee katika dunia nzima. Uelekeo wa sasa utaifanya nchi hii kuwa kinara katika uuzaji madini hayo. Na kwa kufanya hivyo pato la Taifa litaongezeka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alinukuliwa akisema haya kuhusu kudhibiti utoroshwaji wa madini, “Katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi. “Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 kote nchini.”
Aliongeza kuwa masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake.
“Masoko haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya,”alisema Waziri Mkuu.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel, copper, n.k. Aidha, tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana”,alisema Rais Magufuli hivi karibuni wakati akizindua Bunge la 12 jijini Dodoma.
Rais Magufuli alibainisha juhudi nyingine za Serikali kwa kusema:“Kuhusu madini pia, kwenye miaka mitano ijayo pia tutaendelea kuliimarisha Shirika letu la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini; kuwawezesha wachimbaji wetu wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapatia mafunzo, mikopo pamoja na vifaa. Na natambua kuwa, wapo baadhi ya watu wamepewa leseni za utafiti na uchimbaji lakini hawajazifanyia kazi; tutazifuta leseni zao, na maeneo hayo kuyagawa kwa wachimbaji wengine, hususan wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kukuza sekta ya madini.”
Serikali itaendelea kuimarisha masoko ya madini pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini.
Haya yote yanalenga pia kuongeza thamani ya madini na kuongeza ajira hasa kwa vijana zitakazotokana na shughuli zinazohusu madini kama vile uchenjuaji na utengenezaji wa bidhaa za madini
“Tunataka madini yachimbwe hapa Tanzania, yachenjuliwe, yayeyushwe na kisha bidhaa za bidhaa za madini zitengenezwe hapa hapa Tanzania; na ndipo ziuzwe nje ama watu kutoka nje waje kununua bidhaa za madini hapa nchini. Ni imani yetu kuwa, kutokana na hatua tulizopanga kuzichukua sekta ya madini itaweza kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025, alisisitiza Rais Magufuli.
Mchango wa asilimia 10 kwa Pato la Taifa utakuwa mchango wa maana ambao utasaidia katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi mkubwa utakaosaidia kuboresha maisha ya watanzania.