Na. Thereza Chimagu
Wananchi wa Vijiji vya Makong’ondela, Pachani na Kilimanihewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wamepongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko na mitaro wilayani hapo ikiwa ni sehemu ya kufungua fursa za kiuchumi na ukuaji wa miji katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza katika mahojiano maalum hivi karibuni wilayani hapo, wananchi hao walisema uthubutu uliofanywa na Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko mbalimbali utaacha alama ya kihistoria kwa vizazi vijavyo kuhusu wajibu wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Bw. Juma Mazoea Mkazi wa Kijiji cha Makong’ondela ameipongeza Serikali kwa kwa kukamilisha ujenzi wa boksi kalavati lililopo Mto Nalingwenya katika barabara ya Michiga-Makong’ondela na kukiri kuwa kukamilika kwa Kalavati hilo kumerahisisha na kuimarisha mawasiliano na usafirishaji ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo.
“Hapo mwanzo kulikuwa na shida ya usafiri hasa mvua ikinyesha kwani kulikuwa na matope mengi ambayo yalisababisha magari kushindwa kupita na kufanya tulipe nauli ya Shilingi 2000 lakini sasahivi magari yanapita bila matatizo na nauli imepungua tunalipa Shilingi 1000 hivyo imetusaidia kuvusha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Bw. Mazoea.
Naye, Bi. Fatuma Maliki Mkazi wa Kijiji cha Pachani alisema hapo mwanzo walikuwa wanapata shida kuvuka kwenda upande wa pili, lakini hali ni tofauti kwani ujenzi wa daraja hilo umewasaidia wananchi wa vijiji vya Makong’ondela na Pachani kwenda kwenye maeneo yao ya uzalishaji hasa mashambani na si wakulima pekee pia imewasaidia wanafunzi wanaotoka vijiji jirani kuvuka kwenda kwenye Kata yao kwa ajili ya masomo.
Kwa upande wake, Bw. Islam Mahela Mkazi wa Kijiji cha Kilimanihewa ameishukuru serikali kwa kujenga mtaro eneo la sokoni kwani umewasaidia wafanyabiashara kuepukana na usumbufu wa maji kujaa hasa kipindi cha mvua.
“Kabla ya mtaro huu kujengwa wafanyabiashara wa hapa sokoni tulikuwa tunapata usumbufu mkubwa sana wakati wa mvua kwasababu maji yalikuwa yanaingia hadi kwenye maduka lakini tumeona mvua ya juzi kwakweli kuna ahueni maji hayatusumbui tena na tunaahidi kuutunza kwa kufanya usafi ili uweze kudumu”, alisema Bw. Mahela.
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Mwombeki Hussein alisema, TARURA Wilaya ya Nanyumbu imefanya matengenezo ya kawaida ya kuchonga barabara jumla ya Kilomita 442 katika Kata zote 17 wilayani hapo kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi.
“Sisi kama Wakala tumeamua kuzifungua barabara zote zaidi ya km 26 hapa mjini na barabara hizo tumeziwekea vibao vya alama za barabarani kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa barabara hizi, tumezifungua barabara hizi kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi”, alisema Mhandisi Mwombeki.
Mhandisi huyo aliongeza kuwa, mbali na uchongaji wa barabara pia wametekeleza ujenzi wa boksi kalavati moja katika Mto Nalingwenya lenye upana wa mita 4 na kuweka changarawe urefu wa Km 1 Barabara ya Michiga-Makong’ondela ambako kulikuwa hakupitiki kabisa. Pia, wamejenga mtaro eneo la sokoni Kilimanihewa wenye mita 150 na upana kipenyo 0.9 ambao umeshakamilika na wananchi wanaendelea kunufaika.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu unaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani humo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.