MBUNGE WA CHALINZE RIDHIWANI KIKWETE AKUTANA NA WANANCHI WA KATA YA BWILINGU NA KUTEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na wananchi wa Bwilngu

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete ameendelea na ziara yake jimboni hapo kwa kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Bwilingu.

Akizungumza katika kueleza nia ya ziara hiyo amesema kuwa dhamira ya ziara hiyo ni kuwashukuru wananchi kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kura nyingi zilizomfanya Rais Dkt. John Magufuli kuibuka mshindi kwa asilimia 94.7 katika Halmashauri hiyo na pili ni kusikiliza kero za wananchi.

Ad

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Makondomengi, Msolwa Ridhiwani amewahakikishia wananchi juu ya utayari wa serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa Kivuko kutoka Bomani – Msolwa kinachokwamisha shughuli nyingi ikiwemo watoto kushindwa kwenda shule kutokana na mto kujaa maji kipindi cha mvua.

Wakizungumza wananchi hao kupitia hotuba yao walimuahidi Mhe. Mbunge kuwa ujenzi daraja hilo litakapokamilika liitwe kwa jina lake Mbunge jambo ambalo Mhe. Mbunge alilikubali akawaomba liitwe kwa jina la Mrisho Kikwete ili kuenzi Boma la kwanza la mtawala lililojengwa huko Makondomengi.

Aidha, Wananchi hao wa kata ya Bwilingu wameshukuru serikali kwa kuendelea kuzifanyia kazi kero mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo barabara, mikopo kwa vikundi vya maendeleo, migogoro ya wakulima na wafugaji.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Ndugu Nassar Tamim ameiomba Serikali kushughulikia kero za mji wa Bwilingu ikiwemo uhitaji wa barabara za lami, kuboreshwa kwa huduma za afya, kumaliza kero za migogoro ya Ardhi na baraza la ardhi pamoja na kumaliza changamoto ya ukosefu wa umeme katika baadhi ya maeneo.

Akizungumza Mhe. Mbunge amewahakikishia wananchi wa Bwilingu kuwa Halmashauri imejipanga kuboresha mazingira ya usafi na afya kwa mji wa Bwilingu na hasa kwa kuwa mji huo ndiyo sura ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze. Mh. Mbunge aliwahakikishia wananchi kuwa kero au changamoto mbalimbali walizozitaja zitafanyiwa kazi.

Kwa upande wa afya, Mhe. Mbunge ameagiza kuundwa kwa tume kuchunguza malalamiko mbalimbali ya wananchi juu ya kituo cha Afya Chalinze.

“Serikali imeleta fedha nyingi, madawa mbalimbali na watumishi ili kuimarisha utendaji na huduma, kama shida ni wataalamu, upungufu wa madawa ni hatua gani zimechukuliwa hata leo wananchi wanalalamika kuhusu mapungufu hayo. Ndugu Mganga wa Wilaya tunahitaji majibu mara moja ili tujue nini tufanye.” Amesema Mbunge Ridhiwani

Ziara hiyo itaendelea tarehe 2 Desemba kwa Mbunge kuelekea Kata ya Mkange, kupisha sherehe za Siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kimkoa itafanyika Bagamoyo Tarehe 1 Desemba.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mitazamo ya Uongozi ya Mhe. Ummy Ally Mwalimu katika Sekta za Afya, Maendeleo ya Jamii, na Haki za Watoto

Ummy Ally Mwalimu ameonyesha mitazamo ya uongozi yenye mwelekeo wa kujali maendeleo na ustawi katika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *