SEKTA YA VIWANDA NI MUHIMILI KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI

 NA Beatrice Sanga- MAELEZO

 Sekta ya Viwanda ni moja ya sekta zinazochangia pato la Taifa na  kutoa ajira kwa wafanyakazi wengi hususan vijana wanaofanya kazi katika viwanda vidogo na vya kati. Sekta hii ina wajibu wa kukuza viwanda ikiwa ni pamoja na kuongeza ujuzi kwa vijana hawa na  kuleta mabadiriko ya kiuchumi pamoja na kuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ad

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliweka nguvu kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/21-2025 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo utekelezaji huo umehamasisha na kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu kama yalivyoanishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 Ili kuhakikisha sekta hii inachangia na kuleta tija katika uchumi wa Taifa hasa ujenzi wa viwanda mama ( basic industries) na kuimarisha viwanda vilivyopo.

Katika kutekeleza mikakati sekta ya viwanda imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa bidhaa viwandani kama vile viwanda vya kusindika vyakula na matunda, viwanda vya nguo, viwanda vya kusindika pamba, viwanda vya chuma na viwanda vya vifaa vya ujenzi. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda uliowekewa mkazo na Serikali ya awamu ya tano umepelekea ongezeko kubwa la viwanda nchini kutoka viwanda 52,633mwaka 2015 na kufikia viwanda 61,110 mwaka 2020.

Juhudi za makusudi zimeendelea kuchukuliwa katika uongezaji thamani wa malighafi za ndani hususan katika sekta za kilimo, uvuvi, mifugo, maliasili na madini. Hatua hizo zinasaidia kuchangia kuongezeka kwa uzalishaji na mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi na hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kupelekea kukua kwa uchumi pamoja na kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi wa shule, miundombinu, hospitali na upatikanaji wa huduma za maji na nishati

 Mafanikio mengi yaliyopatikana kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ni pamoja na uendelezaji na uanzishwaji wa viwanda vya marumaru, saruji, chuma, vinywaji, na matunda, nyama, maziwa, nguo na mavazi, bidhaa za plastiki na ngozi, hii yote ni katika kuhakikisha viwanda vya ndani vinakua na kuweza kuchangia kukua kwa pato la taifa

Aidha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita sekta hiyo imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo ukuaji wa viwanda na uzalishaji, ukuaji wa shughuli za ujasiriamali, uboreshaji wa mifumo ya ununuzi wa mazao ya wakulima, matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali na matumizi ya fursa za masoko zilizopatikana kutokana na majadiliano ya Kikanda na ya Kimataifa.

Kutokana na mafanikio ya sekta hiyo, ajira mbalimbali kwa Watanzania na wageni kutoka nchi mbalimbali zimeweza kuzalishwa ambapo sekta hiyo imeajiri zaidi ya Watanzania milioni 9 ikiwa ni ya pili katika sekta za kiuchumi ikifuatiwa na sekta ya kilimo

Ajira hizo zimewezesha wahusika kujiongezea vipato na kutatua changamoto zao za kijamii na kiuchumi. Pia, zimeweza kuongeza chachu katika azma ya ujenzi wa viwanda nchini ambapo takribani asilimia 99 ya viwanda vyote nchini vipo chini ya sekta hiyo.

Ukuaji wa sekta hiyo una mchango mkubwa katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati uliotangazwa hivi karibuni na Benki ya Dunia Vilevile, imebeba dhamana ya nchi ya kukua zaidi kwa uchumi unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025, hasa ikizingatiwa kuwa inashirikisha Watanzania wengi katika shughuli za kiuchumi.

Viwanda vingi vilivyoanzishwa vimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya malighafi za Tanzania hususan ongezeko la mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo.

Katika kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi , Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), 2020 imeahidi kujenga na kukuza uchumi shindani hususani kupitia sekta za viwanda na huduma za kiuchumi utakaowezesha ustawi wa wananchi wote.

Kupitia viwanda vidogo vya kati na vikubwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatengeneza ajira zaidi kwa vijana kupitia viwanda vya ndani ambapo itasaidia vijana kuwa na uwezo wa kujikimu na kuchangia katika kuongeza pato la nchi.

Pia Serikali imejipanga kuchochea ukuaji wa uchumi, hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi pamoja na utalii. Hii itapelekea kukuza uchumi wa nchi, kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja, kupunguza umasikini na kuongeza uwezo wa taifa kujitegemea.

Aidha katika miaka mitano ijayo Serikali inaenda kuimarisha mazingira ya ujenzi wa viwanda vya kimkakati kwa kufanya mapitio na maboresho ya sera za mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini( Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Envinroment).

Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *