Akizindua Baraza hilo, Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesema hili ni jukwaa pekee linatoa nafasi ya kukutana na wadau wa sekta binafsi na kujadiliana fursa zakiuchumi ikiwa ni pamoja na utatuzi wa changamoto utakaoleta tija katika mustakabali wa nchi yetu inayosimamia sera ya uchumi wa kati wa viwanda.
Ameongeza kuwa ni chombo kinachoweza kupaza sauti juu ya masuala yahusuyo sekta binafsi na wafanyabiashara kwa minajili ya maboresho yaliyokuwa makwazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema “Ni fursa Muhimu Kama wadau kwakuwa wote tunajenga nyumba moja, tunajenga mustakabali was Nchi yetu, tutakayoyaongea yakajenge Nchi yetu, Tumepata fursa Kama hii tunakwenda kutatua kero zote” Daniel Chongolo.
Akiainisha majukumu ya kamati za baraza hilo la biashara katibu wake kwa niaba ya Mkurugenzi ambaye pia ni Mweka hazina wa Manispaa Ndg Maximilian Tabonwa amesema uundwaji wa Baraza hili ni sehemu ya majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma katika ngazi yaTaifa, Mkoa na Wilaya na kuainisha majukumu hayo kuwa ni kufanya tathmini, kuainisha njia ya utekelezaji wa maboresho, kupendekeza utaratibu wa mfumo, kujadili mahitaji ya rasilimali, kujadili ajenda za mikutano na kufuatilia maombi ya kamati tendaji.
Akijibu changamoto iliyoainishwa na wadau kuhusiana na Tax clearance katika kuhuisha leseni za Biashara, Afisa Biashara wa Manispaa hiyo Ndg.Pastori Magodi amesema ni kwa mujibu wa vifungu vya Sheria vinavyomtaka mfanyabiashara au mtu yeyote anayehuisha leseni kulazimika kushirikiana na TRA, ili kupata taarifa za awali kuhusiana na leseni hiyo kwa maana ya kujua kama anadeni la nyuma au la.
Naye Meneja TRA Mkoa wa Kinondoni Ndg Masawa Masatu alipokuwa akifafanua hoja iliyoelekezwa kwakwe kuhusiana na masuala ya ulipwaji wa kodi, amewataka wafanyabiashara kuwa makini na vishoka na kuhakikisha wanafuata Sheria zinazowapasa katika ulipwaji wa kodi.
Baraza hilo lilipata uwakilishi kutoka Tan Trade, TCCIA, NAKIETE, TRA, Twiga Cement na wafanyabiashara wakubwa na wadogo ambapo walipata nafasi ya kuziainisha changamoto amabzo ni mkanganyiko wa Sheria za Biashara, mwingiliano wa Sheria na majukumu katika utekelezaji, kutokuwepo na uwazi katika taratibu za baadhi ya utekelezaji wa sera katika Biashara, ukiritimba katika kutekeleza Jambo pamoja na mazingira ya biashara kutokuwa rafiki.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Kinondoni amewataka wafanyabiashara wadogo kukuza kipato chao kwa kutumia njia sahihi ikiwemo uchukuaji wa mikopo isiyo na riba katika mkopo wa asilimia kumi kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu.