DC CHONGOLO: JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA MWANANYAMALA KUANZA KAZI BAADA YA WIKI

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Jengo jipya la kisasa la Mama na Mtoto litakalo anza kutoa huduma hivi karibuni.

Akizungumza wakati alipofanya ziara ya kukagua jengo hilo Mhe. Chongolo amesema kuwa jengo hilo ambalo limejengwa kwa fedha za Serikali litakuwa mahususi kwa Wananchi wa maeneo yote yaliopo ndani na nje ya Manispaa hiyo kwa kuwa litatoa huduma nyingi ambazo awali hazikuwepo.

Ad

Ameongeza kuwa kukamilika kwa hatua za mwisho kwa jengo hilo kutatoa fursa ya huduma za ‘CT-SCAN’ pia kuwa na wodi binafsi ‘Privante Room’, kitu ambacho awali hakikuwepo Hospitalini hapo na kwamba Wananchi watapata huduma hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Mhe. Chongolo amesisitiza kuwa mara baada ya kukamilika kwa maandalizi hayo ambayo yatakamilika baada ya wiki mbili, atarejea kuhakiki na hivyo kuruhusu huduma hizo kuanza kutolewa na kwamba Serikali inafanya kazi kubwa katika kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata huduma iliyo bora.

“ Nimefurahishwa na kazi nzuri ambayo imefanyika, ninawapongeza kwa namna ambavyo mnashirikiana kuhakikisha kwamba matumizi ya jengo hili yanaanza rasmi, nitarudi tena kujiridhisha katika maandalizi ya jumla kabla ya kuanza kulitumia hili jengo jipya la huduma ya mama na Mtoto” amesema Mhe. Chongolo.

Aliongeza kuwa anategemea matokeo kwa haraka ili wale ambao wanapata huduma ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala waanze kupata huduma iliyo bora, “”Serikali ya Rais Dk. Magufuli inafanya kazi kubwa, imetoa fedha nyingi kiasi cha Bilioni 2.2 kwa ajili ya Hospitali hii kuboresha huduma inahitaji pia kuona matokeo ya haraka”.

Awali Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Dkt. Nkungu Daudi amempongeza Mhe. Chongolo kwakuwa karibu wakati wa ujenzi wa Hospitali hiyo na kusema kwamba jengo hilo limekamilika kwa asilimia 98 na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni kuunganishwa kwa umeme kwenye jengo pamoja na mfumo wa majitaka wa jamii ili lianze kutumika.

Ameongeza kuwa katika jengo hilo kutakuwa na vitanda, 78 kwa ajili ya watu wazima, Watoto wachanga, Wodi ya Mama na Mtoto,Mama wajawazito, huduma za kujifungulia, sambamba na wale wanaohitaji huduma za kulipia.

“Hospitali hii itakuwa na mambo mengi ya kitaalamu ambayo yapo kwa mfumo wa kisasa zaidi, kutakuwa na utoaji wa huduma za kibingwa ,tuna mabingwa zaidi 24 katika Hospitali yetu ,inawezekana walikuwa wanashindwa kuja kutokana na kukosa huduma hiyo lakini hivi sasa zitakuwepo” amesema Dkt. Nkunga.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *