Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ameahidi kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuboresha mifumo ya hakimiliki ili kuhakikisha wasanii wa mawanda mbalimbali wananufaika kila kazi zao za ubunifu zinapotumika iwe kwenye redio, TV, mitandaoni na kila sehemu ya biashara.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo jioni hii jijini Dar es Salaam alipokutana na waandaaji wa muziki na filamu, Madj na wasambazaji wa kazi za sanaa ikiwa ni mikakati ya pamoja ya kutatua kero za sekta hiyo.
“Tangu Cosota ihamie Wizara ya Habari tumeendelea kuboresha mifumo ya ndani ya kiutendaji ikiwemo kuandaa mifumo mipya ya kimtandao kusajili kazi kiurahisi, kuboresha Kanuni ili wanaokamatwa na kazi za wasanii watozwe faini papo hapo na zaidi tumeiongezea taasisi wafanyakazi na vitendeakazi hasa usafiri na hivi sawa tayari Cosota imeshafungua Ofisi Dodoma. Wasanii wakae tayari kunufaika na mifumo bora zaidi ya kukusanya haki zao,” alisema Dkt. Abbasi.
Katika mikutano hiyo wadau wa sekta ya Sanaa pia wameomba kujengewa kumbi za maonesho na burudani na kupunguziwa utitiri wa kodi ambazo Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amewataka waainishe kodi zenye kero ili zijengewe hoja Serikali.