SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA SHULE ZA UMMA

Na Faraja Mpina – WUUM

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) umetoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 601 wa shule za umma za msingi na sekondari za Tanzania bara na visiwani.

Ad

Mafunzo hayo yametolewa katika makundi mawili ambapo walimu 297 wamepata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na  walimu 304 katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ikiwa ni muendelezo wa Mfuko huo kutoa mafunzo hayo kwa walimu wa umma yaliyoanza kutolewa toka mwaka 2016.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Zainab Chaula amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa  utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 zinazoainisha kuanzisha na kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuboresha mchakato wa ujifunzaji katika viwango tofauti vya elimu.

“UCSAF imegawa kompyuta mashuleni, walimu mnatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanajua kuzitumia, ndio sababu mmepewa mafunzo ili mkatimize wajibu wenu”, alizungumza Dkt. Chaula

Naye Mtendaji Mkuu UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa mfuko huo umekuwa ukipeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu ili kurudisha heshima katika shule hizo.

Amesema kuwa tangu UCSAF ianze kutoa mafunzo hayo mwaka 2016, jumla ya walimu 2,213 wa shule za msingi na sekondari wamepata mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wa kutumia vifaa vya TEHAMA na kufundishia.

Ameongeza kuwa, UCSAF inaendelea kujipanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuendelea kuinua matumizi ya TEHAMA nchini hususani kwa kuwezesha shule za umma.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Elimu Msingi TAMISEMI, Suzan Nusu amesema kuwa walimu waliohudhuria mafunzo hayo walikuwa na vigezo na Wizara itahakikisha mafunzo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa vitendo ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *