KUANZISHWA KWA MFUMO WA KUHIFADHI TAARIFA ZA WAJUMBE WA BODI ZA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA, KUTASAIDIA KUONDOA CHANGAMOTO

Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Neema Musomba akitoa muhtasari wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro, jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wajumbe wa bodi za taasisi na mashirika ya umma, kutasaidia kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa uteuzi wa bodi mpya.

Kwa mujibu wake, serikali ilitoa maelekezo kwa makatibu wakuu na watendaji wakuu wa taasisi za umma kuwasilisha katika mamlaka za uteuzi taarifa za bodi ya taasisi kukaribia kumaliza muda wake miezi sita kabla.

Ad
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana na Dkt Ndumbaro katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Kulia ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka na kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Pili Mazowea. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Maelekezo hayo yalikuwa na lengo la kuhakikisha ndani ya kipindi cha miezi sita, mchakato wa uteuzi wa Bodi uwe umekamilika. Utekelezaji wa maelekezo hayo umekuwa ukisuasua na matokeo yake bado kuna taasisi hazipati Bodi za Wakurugenzi kwa wakati. Naamini kwa mfumo huu unaozinduliwa utaisadia Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na mamlaka za uteuzi kufanyia kazi changamoto hiyo na kuhakikisha Bodi zinateuliwa kwa wakati,” alisema Dk Ndumbaro.

Katibu Mkuu Utumishi aliyasema hayo wakati akizindua mafunzo ya matumizi ya mfumo mpya wa usimamizi wa taarifa za wajumbe wa bodi katika wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma yanayofanyika mjini hapa, na kuandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mwezeshaji katika mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma, Felix Ngoi akitoa mada wakati wa uzinduzi wa hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Hivyo basi, mfumo huu utakua kitendea kazi muhimu cha ofisi yako na naamini hata makatibu wakuu wa wizara wataweza kutumia mfumo huu kupata taarifa za hali ya Bodi zilizo chini ya wizara zao, na kushauri mamlaka za uteuzi mapema iwezekanavyo na hivyo kuondoa changamoto zinazotokana na uchelewaji wa teuzi za Bodi,” aliongeza.

Alieleza kuwa anafahamu kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kuzikumbushia mamlaka za uteuzi kuhusu kumalizika kwa muda wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi za umma na mara nyingi amekuwa akipata nakala za barua hizo.

Mwezeshaji katika mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma, Ntimi Malambugi akitoa mada wakati wa uzinduzi wa hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Aidha, taasisi nyingi za umma zimekuwa zikikaa muda mrefu bila ya kuwa na Bodi za Wakurugenzi. Kutokuwepo kwa Bodi ya Wakurugenzi katika Taasisi husababisha maamuzi mengi katika taasisi hiyo kukwama na kupelekea uchelewashaji wa mambo mengi ya msingi kutofanyika kwa wakati.

“Athari za kutokuwepo na Bodi ya wakurugenzi ni pamoja na kutopitishwa kwa hesabu zilizokaguliwa, watendaji kuendelea kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu pamoja na kuchelewesha stahili mbalimbali za watumishi,” alisema.

Aliongeza, “Hatua za kuimarisha usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi ni za kupongezwa na zinahitajika kuwa endelevu ili kufikia malengo ya kuwepo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina. Nafahamu, ofisi yako haikuwa na mfumo ambao ungeiwezesha kufuatilia uteuzi wa Bodi kwa mamlaka za uteuzi pamoja na taarifa nyingine za utendaji wao.”

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Raphael Chibunda (kulia), akiwaongoza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro (kushoto) na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kuelekea kwenye wa uzinduzi wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoanza jana katika Kampasi Kuu ya SUA, Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Alimpongeza Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kwani utekelezaji wa mfumo huu ni matokeo ya juhudi zinazofanywa na ofisi yake katika kuimarisha usimamizi wa utendaji wa Bodi na Menejimenti za wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taasisi za Umma zinakuwa na Bodi za Wakurugenzi zilizo hai na kupunguza watendaji wakuu wanaokaimu kwa muda mrefu.

Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo wanaofadhili Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa kuwezesha kifedha ujengaji wa mfumo huo na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali katika kuimarisha maendeleo ya nchi.

“Aidha, nawapongeza kwa dhati vijana wetu, Watanzania wenzetu, ndani ya serikali kwa weledi wao na jitihada zao zilizosababisha kufanikisha kujengwa kwa mfumo huu,” alisema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa amefurahi kwa sababu mfumo huo utasaidia kuhakikisha bodi pamoja na watendaji wakuu wanateuliwa kwa wakati.

Washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma wakifuatilia mafunzo hayo yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina).

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema ofisi yake kwa kutumia wataalamu wa ndani ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika mwaka wa fedha 2019/20 pamoja na washirika wa maendeleo ilianzisha Mradi wa Kusimika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za wajumbe wa Bodi za Taasisi za Umma.

Alisema mfumo huu utatumika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, mamlaka za uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi pamoja na wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma katika usimamiaji wa masuala yote yanayohusu bodi hizo.

Mbuttuka alieleza kuwa Mfumo wa Usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi (BMIS) umejengwa na wataalamu wa ndani ili kuhifadhi taarifa za uteuzi wa wajumbe wa bodi, wasifu wao, idadi ya taasisi wanazohudumu, aina za ujumbe wao pamoja kurahisisha utolewaji wa taarifa za bodi kwa wakati.

Alifafanua kuwa mfumo utaisaidia Ofisi ya Msajili wa Hazina na mamlaka za uteuzi kupata taarifa mapema kuhusu bodi kumaliza muda wake, wajumbe wa bodi wanaohudumu katika bodi zaidi ya tatu. 

“Uwepo wa mfumo huu utasaidia kuimarisha usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi za umma kwa kuhakikisha taasisi hizo zinakuwa na Bodi kwa wakati. Mfumo pia utasaidia upatikanaji wa taarifa za uhakika za wajumbe wa Bodi na kwa wakati, ushiriki wao katika vikao na pia itapunguza urasimu wa ufuatiliaji wa uteuzi wa Bodi pale Bodi inapomaliza muda wake. 

Inategemewa kuwa uwepo wa mfumo huu utasaidia sana kuondoa changamoto ya taasisi kutokuwa na Bodi kwa muda mrefu, baadhi ya wajumbe Bodi kuteuliwa katika Bodi zaidi ya tatu, watendaji wakuu kukaimu muda mrefu, usahihi wa taarifa za taasisi kuhusu hali ya Bodi na watendaji wakuu, kuongeza ufanisi wa utendaji wa Bodi na kuzifanya mamlaka za uteuzi kupata taarifa kwa wakati kuhusu hali za Bodi katika taasisi za umma,” alieleza Mbuttuka.

Mafunzo hayo yana washiriki 708 kutoka katika taasisi na mashirika ya umma 236, na watajengewa uwezo wa kutumia mfumo huu. Katibu Mkuu aliwaomba kila mshiriki kuzingatia mafunzo haya kwa umakini na kuhakikisha anauelewa vizuri.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *