SERIKALI YASAINI MKATABA NA KOREA UTAKAOWEZESHA TANZANIA KUPATA MIKOPO YENYE MASHARTI NAFUU

Balozi wa Korea nchini, Cho Tae-Ick akizungumza baada ya kusaini mkataba huo baina ya nchi yake na Serikali ya Tanzania leo jijini Dodoma.

Serikali ya Tanzania imesaini mkataba na Serikali ya Jamhuri ya Korea utakaowezesha kupata mikopo kutoka mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi wa Korea (EDCF).

Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Cho Tae-Ick  ambaye ameambatana na Mwakilishi Mkuu wa mfuko huo wa EDCF Ofisi ya Dar es Salaam, Jo Younkyoung.

Ad

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema serikali ya Tanzania inayo furaha kusaini mkataba huo utakaoiwezesha Tanzania kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka mfuko huo yenye thamani ya hadi Sh Bilioni 684.6 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.

” Fedha hizo zitatuwezesha kutekeleza ujenzi wa vituo viwili vya kupoozea umeme katika njia ya kusafirisha umeme ya Kigoma-Nyakanazi (Gridi ya Taifa ya Kaskazini Magharibi) ambao utagharimu Sh Bilioni 102.9, kusaidia bajeti Kuu ya serikali ambapo Sh Bilioni 91 zitatumika kuziba pengo la kibajeti lililotokana na madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya korona.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James (katikati) na Balozi wa Korea Nchini Cho Tae-Ick (kulia) wakisaini mkataba utakaoiwezesha Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Lakini utatusaidia mradi wa uboreshaji wa huduma za majitaka katika Jiji la Dodoma ambapo Sh Bilioni 160 zitatumika sambamba na kuimarisha miundombinu ya upimaji ramani utakaotumia Sh Bilioni 148 na kiasi cha Sh Bilioni 74 kikisaidia mradi wa ujenzi wa daraja la Salenda,” Amesema Dotto James.

Ametoa shukrani pia kwa ajili ya miradi iliyokwishakamilika ambayo iligharimu Sh Bilioni 542 ambayo pia imefadhiliwa na Korea kupitia mfuko wake huo wa EDCF kwa mikopo nafuu.

Ameitaja miradi ambayo imeshakamilika kuwa ni pamoja ba Ujenzi wa Daraja la Malagarasi na barabara unganishj awamu ya kwanza, mradi wa uanzishwaji wa vituo vya elimu ya ufundi uliokamilika mwaka 2014 na mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Kilimanjaro-Arusha.

Miradi mingine ni ule wa ujenzi wa kituo cha elimu cha Chuo Kikuu cha Muhimbili kampasi ya Mloganzila, mradi wa  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Iringa-Shinyanga pamoja na ujenzi wa vituo vya taarifa za mfumo wa vitambulisho vya Taifa NIDA.

Kwa upande wake Balozi wa Korea Nchini, Cho Tae-Ick ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekua na manufaa kwa watanzania.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *