TARURA YAPONGEZWA UJENZI WA DARAJA LA KANKWALE MKOANI RUKWA

Na. Erick Mwanakulya, Rukwa.

Wananchi wa Kata ya Senga Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa Daraja la Kankwale linalounganisha Sumbawanga Asilia na Kankwale.

Naye, Mkazi wa Mtaa wa Katambazi Bw. Erod Kastiko ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakuwa kiunganishi kikubwa kwa wakazi wa Sumbawanga Asilia pamoja na Kankwale na litarahisisha shughuli za maendeleo pamoja na shughuli za usafiri na usafirishaji.

“Tunaishukuru sana TARURA kwa ujenzi wa daraja hili, hapo awali tulikuwa na daraja lakini kutokana na mvua nyingi, daraja hilo lilisombwa na maji na kusababisha kero kwetu sisi wakazi wa Katamba na vijiji vyote vya jirani, hivyo ujenzi wa daraja hili utatusadia katika suala la usafiri na usafirishaji”, alisema Bw. Erod.

Muonekano wa ujenzi wa Box Kalavati katika Barabara ya Sumbawanga Asilia – Kankwale katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mhandisi Seleman Mzirai alisema kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza mapema mwezi Januari 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari 2021, ila kutokana na kasi ya Mkandarasi ujenzi huo utakamilika mapema mwezi Desemba 2020.

“Ujenzi wa daraja hili umefikia asilimia 70 kukamilika, kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kuta za pembeni ili kuweza kuzuia mmomnyoko wa udongo, daraja hili litasaidia sana wakazi wa maeneo haya katika shughuli zao za usafiri na usafirishaji na hasa kipindi cha mvua kwani litapitika kipindi chote”, alisema Mhandisi Mzirai.

Aidha, mbali na ujenzi wa daraja hilo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetekeleza mradi wa Barabara za Lami zenye urefu wa Km 2.9 ambazo zimekamilika kwa asilimia 100 huku ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Km 1 katika barabara ya Ikulu ambayo ni mradi wa Ahadi za Mhe. Rais ukiwa umekamilika.

Naye, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Mhandisi Elly Jonas Mkwizu alieleza kuwa Mji wa Namanyere kwa sasa unapendeza baada ya kujenga barabara za lami na kwamba mabadiliko yatakuwa makubwa katika Wilaya hiyo baada ya miradi mbalimbali iliyopo katika hatua za utekelezaji kukamilika.

“Namanyere kwa sasa inabadilika, barabara hizi za lami zimeufanya mji upendeze na tunaendelea kuomba bajeti ya kutosha ili tutekeleze miradi mingine walau sehemu kubwa ya mji wetu iwe na barabara za lami”, alisema Mhandisi Mkwizu”.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Mkoa wa Rukwa unaendelea kutatua kero mbalimbali za wananchi kwa kujenga madaraja ili kuunganisha maeneo mbalimbali ya Mkoa huo, ikiwemo ujenzi wa daraja la Kavunja katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ambalo limefikia asilimia 45 kukamilika ili kuunganisha Kata ya Kirando na kata ya Korongwe ikiwa ni pamoja na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo hayo.

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.