Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema atahakikisha utekelezaji wa majukumu ya kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira yanagusa Maisha ya wananchi moja kwa moja kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumza na Menejimenti ya Ofisi yake mara baada kupokelewa rasmi katika Ofisi za Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma hii leo, Waziri Mwalimu amewataka wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo chanya kwa taifa.
Ad
“Tuna jukumu kubwa la kulinda na kuhifadhi mazingira pamoja na kudumisha muungano wetu ambao ni tunu ya Taifa letu” Alisisitiza Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema ni muhimu kuendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa Muungano kwa kushirikisha vijana ambao ni taifa na leo, hususan waliozaliwa baada ya muungano kwakuwa kuna mengi ya kujifunza.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mwita Waitara amesema kuwa atahakikisha kuna kuwa na ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kusimamia kwa pamoja masuala ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira nchini.
Waziri Ummy Mwalimu na Naibu wake Mwita Waitara hii leo wameapishwa rasmi kushika nyadhifa zao mara baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 5 Desemba 2020.