WAZIRI WA MADINI BITEKO AZUIA URASIMU KATIKA SEKTA YA MADINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza jambo wakati wa kikao cha menejimenti cha kumkaribisha rasmi Waziri wa Madini Doto Biteko ofisini tarehe 10 Disemba, 2020 Mtumba Jijini Dodoma.

Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wamekumbushwa kuzingatia maeneo muhimu ya kipaumbele yanayopaswa kutekelezwa kwenye Sekta ya Madini kama yalivyoanishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliyoisoma wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano Novemba, 2020 na Hotuba aliyoitoa Bungeni Mwaka 2015.

Ad

Hayo yamebainishwa Desemba10, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko katika kikao chake na Menejimenti ya Wizara na taasisi zake, baada ya kuteuliwa na kuapishwa tena kuiongoza Wizara ya Madini.

Biteko amewataka viongozi hao kurejea tena maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 ili kuona ni namna gani masuala hayo yametekelezwa huku kila taasisi ikitakiwa kuhakikisha inayafanyia kazi maelekezo yote kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kukua na kuongeza tija kwa taifa ikizingatiwa kuwa, hivi sasa sekta hiyo imeonekana kuwa kichocheo cha ukuaji kwa sekta nyingine kiuchumi.

 Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Doto Biteko (Katikati) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (Kulia), Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula (Kushoto). Kamishna wa Madini David Mulabwa, Wakuu wa Idara, Taasisi na Vitengo kumpokea na kumkaribisha Waziri wa  Madini ofisini tarehe 10, Disemba, 2020 Mtumba Dodoma

Aidha, Waziri Biteko amesisitiza suala la ubinifu ili kuwezesha kuibuliwa kwa miradi mikubwa ambayo itapelekea kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya Tanzania na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye maendeleo na uchumi wa nchi.

Kadhalika, Waziri Biteko amezuia urasimu katika kushughulikia masuala yanayohusu sekta ya madini akilenga kuweka mazingira bora yatakayowezesha biashara ya madini kufanyika kwa ufanisi ili kuwezesha matokeo chanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwemo kuwezesha uwekezaji katika sekta ya madini kufanyika bila kuwepo vikwazo visivyokuwa na sababu.

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa amebeba ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 kama sehemu ya kutekeleza wajibu wa wizara ya kusimamia utekelezaji huo, tarehe 10 Disemba 2020, alipokutana na watendaji wa Wizara ya Madini Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.

‘’ Kama kuna watu wanataka kuchimba wapewe lesni na wapewe fursa na kama kuna maoni yanayohusisha taasisi nyingine basi yafanyiwe kazi haraka. Tuwalee wawekezaji tulio nao ili waendelee kufanyakazi,’’ amesisitiza Biteko.

Ametaka kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayopelekea wafanyabishara na wachimbaji kufanya shughuli zaokwa amani ili kuwezesha kuzalishwa kwa ajira, teknolojia mpya za uchimbaji na uchenjuaji wa madini  vilevile, kuiwezesha sekta kuzalisha mabilionea wengi.

Wakuu wa Taasisi, Idara, Vitengo na watendaji mbalimbali  wa Wizara ya Madini wakimsikilizaWaziri wa Madini Doto Biteko mara baada ya kufika Ofisini Mtumba Jijini Dodoma terehe 10, 2020.

Vilevile, Waziri Biteko ametaka  kufanyiwa kazi suala la utoroshaji wa madini ili kuzuia mianya inayopelekea kutoroshwa kwa madini ambalo ameeleza awali lilianza kufanyiwa kazi vizuri lakini  kwa sasa tabia hiyo imeanza kurejea.

‘’ Mwanzo tulikwenda vizuri lakini sasa tabia hii imeanza kujirudia. Kwenye upande madini feki tumepambana nao na tumekamata mitandao ya watu wa madini feki,’’ amesema Biteko.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ametaka kuhuishwa kwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ili iendane na matakwa ya sasa akirejea Marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini wakimpokea Waziri wa Madini Doto Biteko ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma tarehe 10 Disemba 2020 kwa ajili ya kuanza majukumu yake rasmi.

‘’ Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni ya muda mrefu. Sera hii ianze kuhuishwa haraka ili iandane na matakwa ya sasa kama tulivyofanya kwenye Sheria ya madini ambayo ilitoa nafasi ya kurudisha umiliki wa madini kwa wananchi,’’ amesema Waziri Biteko.

Pia, ametaka suala la kuanzishwa kwa Chama Cha Wajiolojia kupewa msukumo ili likamilishwe haraka ili kuongeza uwajibikaji wa Wataalam hao katika sekta ya madini.

Aidha, katika kikao hicho, Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru watumishi wote wa wizara ya madini na taasisi zake kwa kufanya kazi kwa pamoja kama familia moja na hivyo kuwezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa  katika sekta ya madini.

Waziri wa Madini Doto Biteko akikabishiwa zawadi ya Ua mara baada ya kuwasili Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma tarehe 10 Disemba 2020.
 

‘’ Kuna wakati niliwaeleza kiu yangu ni kujengwa kwa taasisi imara. Nashukuru hata wakati sipo kila taasisi iliendelea kufanya kazi zake vizuri. Kiu yangu ni kuona wizara na taasisi zinafanya kazi kwa pamoja ili tuwatumikie watanzania na tumalize matatizo ya wadau wetu.,’’ amesema Biteko.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amempongeza Waziri Biteko kwa kuaminiwa na kuchaguliwa tena kuiongoza wizara ya madini na hivyo kutumia fursa hiyo kumkaribisha tena wizara ya madini na kueleza ‘’ mafanikio yote yaliyopatikana ni yetu sote kwani sisi sote tulioongea lugha moja,’’.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *