NEMC YAONYWA KUTOKUWA KIKWAZO KATIKA UTOAJI WA VIBALI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kutokuwa kikwazo katika utoaji wa vibali vya mazingira kwa wawekezaji katika kutekeleza miradi ya kimkakati.

Amesema hayo hii leo alipokuwa akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa NEMC mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mikocheni  jijini Dar es Salaam.

Ad
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)

Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na wawekezaji ndani ya nchi juu ya utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ambavyo taratibu zake zinachukua muda mrefu na kusababisha ucheleweshwaji wa maendeleo katika Nchi yetu na kuleta usumbufu usio wa lazima kwa wawekezaji.

“Katika hili nimewaagiza NEMC kuharakisha mchakato wa kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa wakati. Hata hivyo nimebaini kwamba ucheleweshwaji wa vibali hivyo kwa kiasi kikubwa hausababishwi na NEMC bali changamoto kubwa iko kwa wale washauri elekezi ambao ndio wanafanya hizo Tathmini za Athari kwa Mazingira. Kuna haja kubwa kuwasimamia washauri elekezi wa mazingira ambao sio waaminifu. Katika kusimamia hilo tutahakikisha tunaunda kanuni mpya ambazo zitasimamia wataalamu hao” Ummy alisisitiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka mara baada ya kikao kilichofanyika katika Ofisi za Baraza, Mikocheni – Dar es Salaam.

Kuhusu biashara ya chuma chakavu, Mhe. Ummy ametoa muda wa siku 14 kwa Baraza kukutana na taasisi nyingine zinazohusika na biashara hiyo ili kuwa na muongozo bora wa kulinda miundombinu ya umma.

Amebainisha kuwa biashara ya vyuma chakavu imekuwa na changamoto kubwa na kusisitiza haja ya kutoa elimu kwa umma ili kutambua taratibu na mambo ya kuzingatia katika utoaji vibali vinavyotolewa kwa wakusanyaji, wahifadhi na wasafirishaji wa vyuma chakavu.

“Tutakuwa makini zaidi, kuhakikisha biashara ya vyuma chakavu inasimamiwa kikamilifu ili kufikia azma ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, hatutaki biashara hii kuhujumu miundombinu ya Serikali, tutakuwa makini zaidi kuhakikisha vyuma chakavu having’olewi kutoka kwenye mataruma ya reli, alama za barabarani au madaraja” Alisisitiza Waziri Ummy.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi hiyo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy Mwalimu ameagiza uongozi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutumia zaidi Ofisi za Kanda za Baraza ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi badala ya kazi nyingi kufanyika Makao Makuu Dar es Salaam pia ameagiza kuongezwa kwa wataalamu katika ofisi hizo ili kurahisisha utendaji kazi.

Waziri Ummy amesema kuwa Ofisi yake itaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira nchini katika ngazi zote.

“Tumeainisha maeneo makubwa manne ambayo tutayafanyia kazi ili kutunza mazingira. Maeneo hayo ni Viwanda, Migodi, Ujenzi holela katika vyanzo vya maji, pamoja na usimamizi madhubuti wa biashara ya vyuma chakavu” 

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *