DKT. MPANGO AAGIZA WATUMISHI 22 TRA WASIMAMISHWE KAZI

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, amemwagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Dkt. Edwin Mhede kuwasimamisha kazi watumishi 22 wa Mamlaka hiyo wakiwemo baadhi ya Maneja wa TRA wa Mikoa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kujihusha na vitendo vya kifisadi na uzembe kazini vinavyoikosesha Serikali mapato.

Dkt. Mpango alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma, alipokutana katika Kikao Kazi na Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Mameneja wa mikoa wa Mamlaka hiyo, kupanga mikakati namna ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali.

Ad

Aliagiza uchunguzi wa kina ufanyike kwa watumishi hao wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutosimamia ipasavyo matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD), kuwabambikia kodi kubwa wafanyabiashara na kuagiza apatiwe taarifa ya utekelezaji wa maelekezo yake ndani ya siku 90 kuanzia leo.

Dkt. Mpango aliagiza watumishi wafuatao wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi huo. Tanga: Afisa wa TRA Brighton Kasilo, Rukwa: Kaimu Meneja Nkasi Rogers Mkama, Shinyanga: Meneja wa kitengo cha ukaguzi Sara Senso na Meneja wa EFD Kwibin Nyamuhanga, Dodoma: Meneja wa Mkoa Bw. Kabula Mwemezi, Kigoma: Meneja wa Mkoa Jacob Mtemang’ombe, Kasulu: Meneja wa TRA Benward Mwakatundu, Songwe: Afisa TRA Janeth Mlack, na Joshua Daudi Samwel,

Wengine ni Kilimanjaro: Msimamizi wa kituo cha Tarakea Maududi Tingwa, Same: Adam Benta na Adam Ruhusa, Njombe: Maafisa Hilda Samuel Mahenge, Ibrahim Lyndama na Geofrey Mwinuka, Kagera: Meneja Biharamulo Alex Chacha, Ilala: Maafisa Stephen Kauzen, Kimweli, Ngobya, Raphael Meng’alai, Benedict Kasele na Nicodemus Mwandago, na Lindi: Kaimu Meneja Ruangwa, Florian Rubambwa.

“Nakuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Dkt. Edwin Mhede uwapumzishe kazi (relieve them from duty) kuanzia leo kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na umwagize Mkuu wa Idara ya Mambo ya Ndani (internal Affairs) awachunguze wahusika wote ndani ya siku 90 na nipatiwe nakala ya taarifa hiyo ya uchunguzi na hatua zilizochukuliwa dhidi ya kila mmoja wao” Alisema Dkt. Mpango

Vilevile, Dkt. Mpango alimwagiza Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Edwin Mhede, kufanya uhamisho wa lazima wa Maafisa waliokaa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi na kwamba anatambua zoezi hilo litagharimu fedha nyingi lakini ni bora kufanya uhamisho wa watumishi hao kwa kuwa kukaa kwao muda mrefu kwenye vituo vyao kuna athiri utendaji kwa kuwa wengi wao wana mitandao ya kuiba fedha za umma.

Aidha Dkt. Mpango aliiagiza TRA kusimamia kikamilifu matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD) nchini kote na kubaini stakabadhi za kughushi na mashine bandia zinazotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu na pia kutoa muda wa siku 15 kuanzia sasa hadi tarehe 31 Desemba, 2020 kuhakikisha changamoto ya kufutikafutika kwa stakabadhi zinazotolewa na machine hizo za EFD linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Ili uweze kuweka kumbukumbu ni lazima utoe nakala (photocopy) ya risiti kwani usipofanya hivyo baada ya siku chache inafutika. Jamani kwa nini iwe risiti za TRA tu? Mbona kwenye Super Markets wao hazifutiki! Mlishanieleza kuwa sasa mmeanza kusambaza karatasi za risiti ambazo hazifutiki lakini kiuhalisia bado! Hatuwezi kuendelea na utaratibu huo bila kufikia mwisho wake” alionya Dkt. Mpango

Eneo lingine alilotilia mkazo Dkt. Mpango ni hatua ya baadhi ya watumishi wa TRA wasio waaminifu wanaowabambikia wafanyabiashara kodi kubwa na kuzishikilia akaunti zao za Benki na baadae kuwadai rushwa ili wawapunguzie kodi jambo alilosema linawakwaza wafanyabiashara nchini na kuikosesha Serikali mapato.

“Baadhi ya wafanyabiashara hasa wadogo wameanza kukwepa kufanya miamala kupitia benki na kuweka fedha za mauzo benki kwa sababu taarifa za benki (Bank statement) zinatumiwa na TRA kufanya makadirio ya juu mno ya kodi kwa kuangalia ukubwa wa miamala ambayo kwa sehemu kubwa ni fedha za wafanyabiashara wakubwa waliowakopesha bidhaa wafanyabiashara hao. Ninaiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato ikalichunguze eneo hilo ili ukadiriaji wa mapato uwe wa haki  na makadirio hayo yaakisi ukubwa wa biashara.” Alisisitiza Dkt. Mpango

Kuhusu zawadi kwa watoa taarifa za wakwepa kodi, Dkt. Mpango alieleza kuwa kuna malalamiko ya watoa taarifa kutolipwa zawadi zao huku baadhi ya watumishi wa TRA wasio waaminifu wakitoa taarifa zao kwa wakwepa kodi hali ambayo ni hatari kwa usalama na maisha yao na kuutaka uongozi wa TRA kumwandalia taarifa ya mwaka mmoja ya namna walivyowapa zawadi watoa taarifa hao ambao ni muhimu kwa kuwa wanaokoa fedha za Serikali.

Alipiga marufuku TRA kufunga biashara za wafanyabiashara kwa kushindwa kulipa kodi badala yake watumie njia ya kukaa nao na kujadiliana namna ya kulipa kodi hizo na kwamba uamuzi wa kufunga biashara uwe wa mwisho baada ya njia zote kushindikana na mwenye mamlaka ya mwisho ya kufanya hivyo ni Kamishna Mkuu wa TRA.

“Ukifunga biashara ya mtu leo kwa madai ya kodi ambazo anadaiwa za huko nyuma maana yake unapoteza kodi nyingi ambazo ungezipata kama biashara ingeendelea. Kufunga Biashara yawe ni maamuzi ya mwisho kabisa pale inapotokea hakuna mbadala kabisa wa kupata ufumbuzi na nilikwishatoa maelekezo siku za nyuma kuwa uamuzi huo utolewe na Kamishna Mkuu wa TRA in person. Hata matumizi ya Agency Notice busara itumike kumlazimisha mlipa kodi alipe deni – Kimsingi iwe ni njia ya mwisho (last resort) baada ya majadiliano kushindikana kabisa.” Aliongeza Dkt. Mpango

Maeneo mengine aliyoyagusia na kutoa maelekezo ya kuboresha ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa kodi ya majengo, kudhibiti ukwepaji wa kodi kwenye biashara ya vyuma chakavu, kuongeza ukusanyaji wa kodi katika sekta ya madini, kubadilisha nyaraka kutoka lugha ya kiingereza kwenda Kiswahili, kurejesha Imani ya wafanyabiashara kwa TRA na kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kuanzisha Ofisi itakayoshughulikia malalamiko ya kodi kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Bi. Mwanaidi Ali Khamis, amewataka watendaji wa TRA kwenda kwenye maeneo ya wateja wao na walipa kodi kwa ujumla badala ya kukaa maofisini wakisubiri kuletewa mapato ili malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli atimize ndoto zake za kuiletea nchi maendeleo.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, alimhakikishia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kuyafanyiakazi ipavyo maelekezo yote aliyopewa kwa moyo mkunjufu na kwa tathimini kubwa aliyoifanya kuhusu utendaji wao na kwa kikao hicho alichokiita ni cha kistoria.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Makamu wa Rais Dkt. Mpango Awakaribisha Wawekezaji Katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *