Serikali ya Rwanda imeeleza kuridhishwa kwake na utoaji wa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam na kuahidi kuendelea kuitumia Bandari hiyo ambayo inahudumia zaidi ya asilimia 80 ya mizigo ya Nchi hiyo.
Balozi wa Rwanda hapa Nchini Meja Jenerali Charles Karamba ameyasema hayo mjini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa Tanzania na Rwanda si nchi jirani pekee bali ni ndugu wa damu na kwamba Rwanda inaiona bandari ya Dar es Salaam kama bandari ya Rwanda
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi kwa upande wake amesema Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara kwa nchi jirani na nyingine zinazoitegemea Tanzania kupokea na kusafirisha mizigo yake ambapo Tanzania imekuwa ikitumia ndege za Rwanda kusafirisha minofu ya samaki nje ya nchi wakati ikijipanga kununua za kwake ili kuongeza kasi ya biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki
Katika mazungumzo hayo pia Balozi Meja Jenerali Charles Karamba ameitumia fursa hiyo kumfahamisha Prof. Kabudi juu ya uwepo wa mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya za Madola (CommonWealth) unaoatarajiwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu nchini Rwanda ambapo itakuwa fursa nzuri zaidi kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara kutokana na uwepo wa mkutano huo.