TARURA WAHIMIZWA KUONGEZA KASI YA UTENDAJI KAZI

Na. Erick Mwanakulya.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Festo S. Dugange ameutaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuongeza kasi ya uboreshaji miundombinu ya barabara na madaraja na kushughulikia kwa wakati athari zinazotokea za uharibifu wa miundombinu hiyo kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.

Ad

Dkt. Dugange aliyasema hayo alipotembelea Ofisi za TARURA Makao Makuu jijini Dodoma kwa lengo la kukutana na Uongozi wa TARURA kwa madhumuni ya kujitambulisha na kupata taarifa ya majukumu na utendaji wa TARURA.

“Sote tunafahamu umuhimu wa Sekta ya Barabara ni kiungo muhimu cha uchumi wa wananchi wetu, TARURA tumepewa sekta nyeti ya kuchangia uchumi katika nchi yetu, tunahitaji kuona kasi tuliyokuwa nayo Miaka Mitatu iliyopita inaongezeka zaidi, hivyo katika maeneo machache ambayo hayafanyi vizuri tuongeze nguvu ya kusimamia kwa ukaribu zaidi ili wananchi waliotupa dhamana hii waweze kuona malengo ya uanzishwaji wa TARURA yanaendana na dhamira ya Rais wetu”, alisema Dkt. Dugange.

Dkt. Dugange amemtaka Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff kuhakikisha kila mradi wa Barabara unaosainiwa utekelezwe ndani ya kipindi cha mkataba, na kuongeza kuwa hatokubaliana na utaratibu wa kuongeza muda wa mikataba kwa Wakandarasi kama hakuna sababu za msingi.

“Kumekuwa na changamoto ya mikataba kutotekelezwa kwa wakati, mikataba inasainiwa lakini haimaliziki kwa wakati, hivyo tunalazimika kuongeza muda wa utekelezaji wake jambo ambalo linaongeza gharama, linapunguza thamani ya fedha na kupunguza ufanisi wa malengo ya Serikali, hivyo basi ni vyema mikataba yote ya ujenzi wa barabara ikazingatia masharti yaliyopo kwenye mikataba ili kuondoa changamoto hii”, alisema Dkt. Dugange.

Aidha, Dkt. Dugange alitoa rai kwa Wakandarasi watakaopata kazi za TARURA kuhakikisha wanazingatia mikataba yao na kusisitiza kuwa Serikali haitakuwa tayari kuona mikataba inapita muda wake wa utekelezaji na amewataka kutekeleza miradi hiyo kwa viwango na ufanisi unaotakiwa ili kuendana na thamani ya fedha.

Pia, Dkt. Dugange ameipongeza TARURA kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneno mbalimbali nchini, kwani utendaji kazi umeongezeka lakini pia ufanisi na thamani ya fedha katika ujenzi wa barabara umeongezeka na kuahidi kusaidia katika utatuzi wa changamoto ya uhaba wa watumishi ili kuongeza ufanisi zaidi.

Pia, ameipongeza TARURA kwa kuimarisha na kuboresha mahusiano na Watendaji ngazi ya Halmashauri na kuongeza kuwa, siku za nyuma hakukuwa na mahusiano mazuri na Watendaji ngazi ya Halmashauri kwani baadhi ya maeneo Wakurugenzi na Madiwani walikuwa hawashirikiani na Watendaji wa TARURA katika kutatua changamoto za wananchi, lakini Mtendaji Mkuu amelisimamia hilo na Watendaji wa TARURA katika Halmashauri wanahudhuria vikao vya Madiwani na wanashirikiana kwa karibu na watendaji hao.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff alimuelezea Naibu Waziri huyo kuwa Wakala unakabiliwa na ufinyu wa bajeti na kuwa kiasi wanachopata kwa sasa ni sawa na asilimia 27 ya mahitaji halisi na kueleza kuwa wataendelea kuboresha miundombinu kwa ufanisi kwa kutumia kiasi hicho wanachopata.

TARURA inasimamia Mtandao wa Barabara za Wilaya (barabara za vijijini na mijini) wenye jumla ya Km 108,946.19 ambapo kati ya hizo Km 2,250.69 ni za lami, Km 27,809.26 ni za Changarawe na Km 78,886.25 ni za Udongo. Jumla ya Km 576 zimejengwa na kukarabatiwa kwa kiwango cha lami, Km 1,538 zimejengwa na kukarabatiwa kwa kiwango cha Changarawe, na zaidi ya Km 35,000 zimefanyiwa matengenezo. Jumla ya Madaraja makubwa 7 yenye urefu wa zaidi ya Mita 20 (span) na madaraja madogo 225 yenye urefu wa mita chini ya 20 yamejengwa.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Makamu wa Rais Dkt. Mpango Awakaribisha Wawekezaji Katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *