WAZIRI JAFO ATANGAZA WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2021

Na. Majid Abdulkarim

Jumla ya wanafunzi 759,706 sawa na asilimia 91.1 ya wanafunzi waliofaulu wakiwemo wavulana 368,174 na wasichana 391,532 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.

Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo wakati akitoa taarfa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021 leo jijini Dodoma.

Akizungumza Mhe. Jafo amesema kuwa kati ya wanafunzi 4,169 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni ambapo wanafunzi 970 watajiunga na shule za wanafunzi wenye ufaulu mzuri Zaidi.

Pia Mhe. Jafo amesema kuwa wanafunzi 1,238 watajiunga na shule za ufundi, wanafunzi 1,961 watajiunga na shule za bweni za kawaida.

Wanafunzi 755,537 wakiwemo wavulana 362,247 na wasichana 385,665 wamechaguliwa kujiunga na shule za Sekondari za kutwa katika maeneo mbali mbali nchini.

“Miongoni mwa waliochaguliwa, wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 2,491 wakiwemo wavulana 1,312 na wasichana 1,179 sawa na asilimia 75.0 ya wanafunzi wenye ulemavu waliofanya mtihani huo.
Mhe. Jafo ameeleza kuwa jumla ya mikoa tisa ya Kagera, Katavi, Lindi, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Songwe na Tabora imeweza kupangia shule wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.

Hata hivyo jumla ya wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9wakiwemo wavulana 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

“Hivyo wanafunzi wenye sifa ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii ya kwanza watapangiwa shule katika awamu ya pili kabla ya tarehe 28 Februari, 2021”, ameeleza Mhe. Jafo

Kwa kuongezea Mhe. Jafo amesema kuwa wanafunzi hao wataendelea kupangiwa shule kadri Mikoa na Halmashauri zitakavyoendelea kukamilisha vyumba vya madarasa na madawati hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2021.

Aidha amewaagiza walimu na watendaji wa sekta ya Elimu katika ngazi zote kuongeza bidii katika usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu ili kufikia malengo ya elimu yaliyopangwa na serikali.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *