WAZIRI MHAGAMA AWAASA WAFANYAKAZI OSHA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WELEDI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) pamoja na wajumbe wa meza kuu wakiimba wimbo wa Umoja na Mshikamano wakati wa Mkutano wa Baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewaasa wafanyakazi wa  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi ili kuwa na tija katika kuchangia uchumi wa kati.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wakala hiyo uliofanyika tarehe 17 Desemba, 2020 Mkoani Morogoro kwa kuzingatia ni chombo muhimu kwa watumishi kukutana kujadili masuala muhimu ya taasisi yao na kufanya maamuzi.

Ad

Waziri Mhagama alieleza ipo haja ya kila mtendaji katika Taasisi hiyo kuona umuhimu wa kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuzingatia mchango unaotolewa na OSHA katika kulifikisha Taifa katika uchumi wa kati kwa kuzingatia majukumu yake ya msingi.

“Jitihada za OSHA katika kutekeleza majukumu yake zina mchango mkubwa kuendeleza uchumi wa viwanda na kuboresha mazingira ya biashara na Uwekezaji nchini na ni ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, ya kukuza viwanda,”alisema Waziri Mhagama.

Aliongezea kuwa, kuwe na jitihada za makusudi za kila mfanyakazi kutambua umuhimu wa kubadili mitazamo hasa kiutendaji kwa kuondokana na mazoea na kuendana na kasi ya Awamu hii.

“Hatuna budi kubadilika kifikra na hasa katika utendaji wa kazi zetu za kila siku.  Tuepuke kufanya kazi kama tulivyozoea zamani pamoja na ufinyu wa rasilimali fedha uliopo hivyo Menejimenti tunatakiwa kujipanga ipasavyo kusimamia upatikanaji wa haki za wafanyakazi na wafanyakazi kutimiza wajibu wao,” Alisisitiza

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Bi. Khadija Mwenda alieleza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa katika ofisi yake ili kuhakikisha wanaendelea kuwa na matokeo chanya ni pamoja na; Marekebisho ya sheria kuhusiana na tozo na ada, kuondoa urasimu, usimikaji wa mfumo wa tehama, uratibu wa ukaguzi kupitia makao makuu ya taasisi/kampuni na kuongeza uwajibikaji.

“Wakala umeongeza uwajibikaji na kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuanzisha dawati la kushughulikia kero na malalamiko mbali mbali ya wadau pamoja na kuazishwa kwa utaratibu wa wakaguzi wake kufanya kaguzi kwa timu badala ya mkaguzi mmoja mmoja ambapo itaongeza uwazi katika ukaguzi na hivyo kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji huduma na kuondoa usumbufu,”alisema Khadija

Alimalizi kwa kuitoa hofu jamii kuwa, watatekeleza maelezo ya Waziri pamoja na kuhakikisha wanaondoa urasimu katika utoaji huduma hasa katika yale maeneo yenye viashiria hivyo ikiwemo, muda wa kupata cheti cha Usajili sehemu ya kazi pamoja na kupunguza muda wa kushughulikia kutoka siku 14 hadi siku 1 baada ya mwombaji kukamilisha mahitaji yote ya usajili na kutoa leseni ya Kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya Mahali pa Kazi kutoka siku 28 hadi siku 3 baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *