WAZIRI LUKUVI ANEEMESHA VIJIJI VITATU KWA KUVIPATIA EKARI MIA TATU SAME

Na Munir Shemweta, SAME


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameshusha neema kwa vijiji vitatu vya Ndungu, Msufini na Mpirani vilivyopo tarafa Ndungu wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa kuvipatia ekari mia tatu vijiji vitatu.

Ad


Hatua hiyo inafuatia wananchi wa vijiji hivyo kuomba kupatiwa sehemu ya ardhi ya Mwekezaji ambaye ni kampuni LM Investment inayozalisha Katani kutokana na ardhi ya maeneo wanayoishi kuwa tepetepe ambapo baada ya uamuzi huo sasa Mwekezaji atabakia  na ekari 2,452.844.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akisisitiza jambo mbele ya wananchi wa Tarafa ya Ndungu wilayani Same baada ya kuwatangazia kupata ekari mia tatu katika vijiji vya Msufini, Mpirani na Ndungu tarehe 20 Desemba 2020.


Akizungumza na wananchi wa Ndungu wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro tarehe 20 Desemba 2020 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema,  baada ya Mwekezaji kuachiwa ekari hizo 2,452.844 serikali inachotaka  ni kuona uwekezaji ukifanyika kwenye shamba hilo na kinyume na hivyo Mwekezaji atanyang’anywa shamba. 


Alimuonya Mwekezaji LM Investment ahakikishe anaendeleza  shamba lake  na kupanda mkonge ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana na kusisitiza kuwa haiwezekani Mwekezaji kuwa na ekari 2,452.844 halafu atoe ajira ya watu 50 tu. 


“Hatufukuzi wawekezaji bali tunataka maendelezo katika shamba na tunataka muwekezaji kuacha kutumia mkopo kuendeleza maeneo mengine” alisema Lukuvi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifurahiwa na wananchi wa Tarafa ya Ndungu wilayani Same baada ya kuwatangazia kupata ekari mia tatu katika vijiji vya Msufini, Mpirani na Ndungu tarehe 20 Desemba 2020.


Ombi la wananchi hao kutaka kumegewa ardhi ya shamba la Mwekezaji lilisababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuona umuhimu wa wananchi hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya makazi na kuamua kupunguza sehemu ya ardhi la  shamba la Mwekezaji na kukipatia kila kijiji ekari mia moja.


Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, tayari taratibu zote za upimaji na upangaji wa eneo la shamba hilo zimefanyika ikiwemo kusajili ramani na kuweka wazi kuwa wiki hii ofisi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Same itakwenda kukabidhi ardhi kwa vijiji hivyo vitatu pamoja na Mwekezaji . Waziri Lukuvi alisema, sasa ardhi ya shamba hilo imehama kutoka mikono ya kijiji na sasa wananchi wake watapatiwa hati za mjini za miaka 99 na Hati za Kikila hazitatolewa katika eneo hilo  kama ilivyokuwa ikifanyika huko nyuma.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua uzalishaji katani katika shamba là Mwekezaji LM INvestment Tarafa ya Ndungu wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro alipokwenda kuvipatia vijiji vitatu ekari mia tatu kwa ajili ya makazi tarehe 20 Desemba 2020, kulia kwa Lukuvi ni Mkuu wa wilaya ya Same Rosemery Senyamule.


” Halmashauri na serikali ya kijiji mtakaa pamoja na kukokotoa gharama za kuchangia maana  tumefanya kazi kubwa ya kuwatafutia ardhi na gharama zenyewe hazitazidi zile za mjini, pamoja na eneo hilo kupangwa lakini eneo ambalo wananchi walijenga muda mrefu nalo litarasimishwa” alisema Lukuvi.


Akigeukia suala la ukaguzi mashamba, Lukuvi aliagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba yote makubwa kwa lengo la kutaka kujua uwekezaji uliyofanyika pamoja na kujua namna Wawekezaji  yanavyochangia kodi za serikali  pamoja na utoaji ajira kwa wananchi wanaozunguka mashamba hayo.


Waziri Lukuvi aliagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi katika mikoa  kufanya ukaguzi haraka na kuona kama uwekezaji wa mashamba makubwa kama una tija.


Kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo  Mzee Kabongo mkazi wa Ndungu  alimshukuru Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwezesha kupatikana kwa ekari hizo mia tatu kwa vijiji vitatu  na kumuomba Waziri Lukuvi kufikiria uwezekano wa kuongeza ekari nyingine katika vijiji hivyo. 

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *