DKT. GWAJIMA AMETAKA PESA ZA DAWA ZIHESHIMIKE

Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya vya umma wametakiwa kuheshimu fedha za dawa kadri zilivyopangwa kwenye bajeti ya Serikali kuu na vyanzo vingine  ili kuweza kuondoa kero ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya nchini.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima  wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 21 wa kutathimini utekelezaji wa vipaumbele vya kisera katika sekta ya afya uliofanyika jijini Dodoma.

Ad
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima akifungua mkutano wa 21 wa kutathimini vipaumbele vya utekelezaji wa kisera katika sekta ya afya uliofanyika jijini Dodoma

Dkt. Gwajima amesema kuwa bado kuna maoni mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini,hivyo viongozi wa hospitali na vituo vya kutolea huduma vya umma wanapaswa kuanisha matumizi ya fedha za dawa walizopokea au kutoka kwenye makusanyo ya mapato ya hospitali hiyo Pamoja na matumizi yake.

“Ili kufikia azma ya Mhe. Rais, sisi kama sekta ya afya inabidi kuongeza kasi katika uwajibikaji wa Pamoja katika malengo tuliyoyaweka, ni lazima tufanye upekuzi wa matumizi ya fedha za dawa,vifaa na maabara lazima ziheshimike na kufika kwa mgonjwa  ili wananchi watuamini na kuweza kutatua kero zao”. Alisema

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiongea na washiriki wa mkutano huo(hawapo pichani) ambapo alisistiza uwajibikaji kwa viongozi katika kuwatumikia wananchi

Aidha, Dkt. Gwajima  amesema katika kutekeleza hilo,Wizara  itatoa maelekezo ya kuongeza ufanisi katika uwajibikaji kuanzia kwa watumishi wote wa sekta ya afya,ngazi mbalimbali za usimamizi na uendeshaji katika sekta na taasisi zilizo chini ya wizara Pamoja na wadau wote wanaotekeleza masuala mbalimbali katika sekta ya afya.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amewahimiza  wadau wote kuweka kipaumbele kwenye utekelezaji kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na serikali kwa miaka mitano ijayo (2020-2025),kwa uwajibikaji wa Pamoja katika ngazi zote za kutolea huduma za afya nchini na hivyo kuboresha  huduma zitakazotolewa ili kuwafikia wananchi wote na kuwapatia huduma kulingana na mahitaji ya kiafya yanayowakabili.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange akiongea kwenye mkutano huo ambao umewakitanisha viongozi mbalimbali kutoka wizara ya afya,TAMISEMI,Wizara zinazojihusisha na masuala ya afya,sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo nchini.

Aliongeza kuwa licha ya mafanikio ya sekta ya afya nchini ,sekta hiyo bado inaendelea kuwa na changamoto  ambazo juhudi za Pamoja zinahitajika  ili kukabiliana nazo ikiwepo ile ya wananchi wengi bado wako nje ya mfumo wa bima ya afya  na hivyo kukosa huduma za afya kwa wakati kutokana na changamoto za kifedha ambapo hadi sasa ni asilimia 11 tu ndio wamejiunga.

Kwa upande wa tiba asili na tiba mbadala Dkt. Gwajima amesema zimekuwa zikisaidia katika kutibu magonjwa mbalimbali  kwa wananchi na hivyo serikali inakusudia kuimarisha  kitengo cha utafiti  wa tiba mbadala.

Waziri Dkt.Gwajima akimkabidhi tuzo ya shukrani Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Afya Edward Mbanga.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema ili kufikia lengo la kuwawezesha  wananchi wote kuwa na bima ya afya  kunahitajika kuimarisha kwa mifuko ya bima ya afya na ili  kuwafikia wananchi wengi zaidi ni kuweza kukamilisha mpango mkakati wa sera ya ugharamiaji wa huduma za afya  Pamoja na sheria ya bima kwa wote.

“Mfuko wa afya  ya jamii ulioboreshwa kwa sasa unachangia asilimia  5 ya wanufaika  wote waliojiunga  katika mifuko ya bima za afya nchini na katika kipindi cha utekelezaji wa mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa  kuanzia Julai 2018 tumefanikiwa kusajili kaya 557,882 sawa na wanufaika 3,347,112 kufikia Novemba 2020”. Alisema Dkt. Dugange.

Wakurugenzi wa taasisi zilizo chini ya wizara ya afya wakifuatilia mkutano huo ambapo wametakiwa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa afya ili kuimarisha huduma za afya nchini

Hata hivyo amesema jumla ya shilingi bilioni 16.2 zimekusanywa katika kipindi  cha mwaka 2018 hadi 2020 ambapo zimewezesha  kuimarisha huduma  za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwawezesha wananchi yakiwemo makundi maalum kuzifikia  huduma hizo  bila vikwazo vya kifedha.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa afya Dkt. Godwin Mollel amesema upo uwezekano wa sekta ya afya kufanya vizuri endapo viongozi na wadau wa maendeleo wakijipanga na kushirikiana  ili kufikia malengo ya kuwahakikishia watanzania wanapata huduma za afya bora na  kwa uhakika.

Katika mkutano huo watendaji wakuu wa sekta ya afya walisaini mkataba wa kisera ambao utatekelezwa na wadau wote nchini

Dkt. Mollel amesema matatizo na kero nyingi ambazo zipo kwa wananchi zinahitaji uelewa kwani wananchi wengi bado hawajafikiwa na hii ni kutokana na mfumo wa mawasiliano,hivyo amewata waganga wakuu wa Mkioa,Wilaya na waganga wafawidhi wa hospitali kutoa mawasiliano yao ili wananchi waweze kusaidiwa pale pasipohitaji msaada.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *