LUKUVI AAGIZA CHUO CHA ARDHI MOROGORO KUTAFUTA GHARAMA HALISI YA URASIMISHAJI MAKAZI

Na Munir Shemweta, ARUSHA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemuagiza Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala kukokotoa gharama halisi za uendeshaji zoezi la urasimishaji ili aweze kupanga bei ya urasimishaji anayopaswa kulipa kila wananchi.

Lukuvi ametoa agizo hilo tarehe 21 Desemba jijini Arusha alipokwenda katika mtaa wa Muriet kukagua zoezi la urasimishaji makazi linalofanywa na chuo cha ardhi Morogoro (ARIMO).

Ad

Alisema, wakati chuo hicho cha Ardhi Morogoro  kikiendesha zoezi la urasimishaji kwenye mitaa ya Mlimani, FFU, Msasani na Muriet  jijini Arusha ni vyema chuo hicho kikatumia zoezi hilo kama shamba darasa kwa kukokotoa gharama halisi ili kujua kiwango anachopaswa kuchangia mwananchi kwa kuwa makampuni binafsi hayawezi  kuweka viwango halisi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua Mawe ya Mipaka (Vigingi) vinavyojengwa na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kwa ajili ya zoezi la urasimishaji makazi katika Kata ya Muriet jijini Arusha tarehe 21 Desemba 2020 alipokwenda kukagua zoezi hilo.

“Hii  mitaa minne mliyopewa kurasimisha mfanye ukokotoaji wa uhakika kujua gharama halisi ili baada ya mwisho wa mwezi Januari mtakapokamilisha kazi hiyo nitangaze viwango halisi na mkisema  gharama ni 50,000 nitatangaza kiwango hicho” alisema Lukuvi.

Kwa sasa kiwango cha  mwisho kilichotangazwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ambacho mwananchi anayerasimishiwa eneo lake ni 150,000.

Kwa mujibu wa Lukuvi,  awali kila kampuni ilijiwekea kiwango chake na  yeye baada ya kuona viwango holela vilivyofikia hadi shilingi laki nne aliamua kushusha mpaka 150,000 na kubainisha kuwa hakuna kampuni iliyolalamikia ushushaji huo na kusisitiza kuwa mara atakapoelezwa kiwango halisi basi gharama halisi kumrasimishia mwananchi kwa nyumba moja itajulikana.

Amewahakikishia wananchi wa Muriet kuwa, baada ya kukamilika zoezi la urasimishaji watakuwa wametoka kwenye makazi holela na kuingia  kwenye makazi rasmi ingawa awali wananchi hao walivunja sheria kwa kujenga kiholela na ndiyo maana serikali imewaomba kuchangia zoezi la  kurasimishiwa na kuwataka  kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuwatimizia wajibu wa kuingia kwenye makazi rasmi.

Alisema, baada ya kurasimishiwa makazi na maeneo yao kupangwa  kutakuwa na faida kubwa  ikiwemo upatikanaji miundo mbinu na huduma nyingine za kijamii zitakazosimamiwa na Mkurugenzi wa halmashauri na kuongeza kuwa wajibu wa wananchi katika kata ya Muriet ni kuchangia 150,000 ili wamilikishwe.

Alibainisha kwa kusema kuwa, wakifanya urasimishaji wanakuwa na mitaji iliyo hai na siyo mfu kama ilivyokuwa kabla ya urasimishaji na kueleza kuwa hati ya umiliki ardhi itawawezesha wananchi kuwa na  usalama wa miliki ya ardhi na kuwaliwataka watendaji wa jiji la Arusha kupita kwenye mitaa kuwahamsisha wananchi kurasimisha maeneo yao

Lukuvi alisema, ni vigumu wananchi kuchangia kwa pamoja na kwa wakati mmoja na kutoa wito kwa mabenki kutafuta namna ya kushiriki zoezi hilo kwa kuwakopesha wamiliki 150,000 na kurejesha kiasi hicho wakati wa kuchukua hati ili zoezi hilo liende kwa kasi.

Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala alimueleza Waziri Lukuvi kuwa, chuo chake kilianza zoezi la urasimishaji katika mtaa wa Muriet Juni mwaka huu na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo mwishoni mwa mwezi Januari 2021.

Kwa mujibu wa Lugala, katika kuhakikisha kazi hiyo inakamilika haraka na kwa wakati wameamua kutumia wanafunzi wa chuo cha Ardhi Morogoro sambamba na kufyatua mawe ya mipaka ( vigingi) wenyewe ambapo kwa siku chuo chake kinafyatua vigingi 160 na kuahidi kuendelea kuongeza idadi na kufikia 200 kwa siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Kimanta alitumia fursa kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuwasamehe wananchi waliojenga kiholela ambapo baada ya zoezi la urasimishaji sasa watatambulika.

Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuanzisha Ofisi ya Ardhi ya mkoa na kueleza kuwa uanzishwaji ofisi hiyo umeongeza uwekezaji  katika huduma nzima za ardhi na kusisitiza kuwa  ataendelea kuiunga mkono ofisi hiyo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *