Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini
Dkt.Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA – CCC akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Andrea Kundo Mathew kwa malengo ya kukutana na bodi, menejimenti na wafanyakazi wa taasisi za Wizara yake ili waweze kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuweka mwelekeo wa utendaji kazi wenye matokeo ili kufikia matarajio na ndoto za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuunda Wizara hii mpya
Amesema kuwa wananchi wana malalamiko kuhusu huduma wanazozipata hususani kwenye mitandao ya simu kuhusiana na mabando yao kuisha, kubadilishiwa gharama za matumizi ya mabando, kupunjwa mabando yao na fedha wanazotuma kwa njia ya mtandao na haya yote yanahitaji majibu na kupatiwa matibabu
“Hatutaki kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato, tutakwenda kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate taarifa ya malalamiko mangapi yamepokelewa, mangapi yamefanyiwa kazi, mangapi yameisha na kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua changamoto za wananchi,” amesisitiza Dkt. Ndugulile
Ameongeza kuwa ni vema tuweke mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za mawasiliano na bidhaa za TEHAMA na taarifa na siri zao kwa kuwa sekta hii inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi madukani na tumieni lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia huduma na bidhaa za TEHAMA na muwe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Baraza ili kutekeleza sheria ya TCRA iliyounda Baraza
Katika hatua nyingine ameitaka Tume ya Taifa ya TEHAMA kuishauri vizuri Wizara ili kufahamu mwenendo na mwelekeo wa wapi tunataka tupeleke TEHAMA ndani ya nchi na tujue tuna wataalamu wangapi wa TEHAMA, tunahitaji wataalamu wa namna gani na waje watibu changamoto za aina gani.
“Tumejiwekea malengo ya kuhakikisha kuwa matumizi ya brodibandi yanafikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 45 ya mwaka 2020 ili wananchi wanufaike na huduma za mawasiliano”, amefafanua Dkt. Ndugulile
Naye Naibu Waziri, Mhandisi Kundo Andrea Mathwe ameongeza kuwa TCRA na TCRA CCC ni taasisi zilizo chini ya Wizara na moja inashughulika na watoa huduma na nyingine watumiaji wa huduma ambapo ni rahisi kufanya nao kazi na kuishauri Wizara kutatua malalamiko ya wananchi kwa kuwa mwananchi anaweza kulalamika kuwa ameibiwa bando kumbe akielemishwa atafahamu vizuri kwanini bando limeisha na hii itawafanya wananchi wavutiwe zaidi kutumia huduma za mawasiliano na hatimaye tutachangia pato la taifa ili kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025
Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shao Msuya amesema kuwa Baraza limejipanga kushughulikia maelekezo yaliyotolewa kwa kuwa watumiaji wa huduma na bidhaa za TEHAMA wameongezeka tofauti na mwaka 2003 wakati Baraza linaanzishwa ambapo kulikuwa na huduma chache ya kupiga na kupokea simu na za vifurushi tu wakati hivi sasa kuna huduma za kutuma na kupokea pesa, tutaongeza kasi ya utendaji kazi ili twende na kasi ya ukuaji wa TEHAMA nchini
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA amesema kuwa watazingatia suala la usajili wa wataalamu wa TEHAMA pamoja na maeneo yao ya ubobezi ikiwemo usalama wa mtandao; utengenezaji wa programu; uchakataji na uhifadhi wa taarifa na data; na ubunifu ili nchi iwe na wataalamu wa kutosha na kuendana na mahitaji kwa kuzingatia kasi ya ukuaji wa TEHAMA duniani
Dkt. Ndugulile ataendelea na ziara yake kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambapo atazungumza na bodi, menejimenti na wafanyakazi