Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Wataalam wa Maabara nchini wametakiwa kuongeza kasi katika kuhakikisha huduma za tiba inayotolewa inafuata miongozi ya wizara na kuhakikisha wanabadili fikra na mitazamo ili kuwafanya wateja wao waweze kuvutiwa na huduma wanazozisimamia.
Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame wakati wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.
Dkt. Mhame amesema kuwa miongozo hiyo itakayowasilishwa kwa siku mbili imesisitiza kuboresha utoaji wa huduma za tiba pia masuala ya usimamizi wa huduma za damu salama pamoja na sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia Tiba Asili nchini.
“Hakikisheni masuala haya ambayo ni mtambuka katika utoaji wa huduma mnayaelewa vyema ili muweze kuisaidia jamii, ikumbuke kuwa yapo maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa hususan suala la tiba asili na tiba mbadala hivyo muhakikishe mnawawezesha waratibu hao pindi inapotokea changamoto katika kusimamia huduma hizi kwenye ngazi mnazosimamia”.Alisisitiza Dkt. Mhame.
Hata hivyo Dkt. Mhame aliwataka washiriki hao kuhakikisha ujumbe utakaotolewa kwenye kikao kazi hiko kitawafikia walengwa ili pindi ukaguzi na usimamizi shirikishi utakapofanyika uwe na tija katika kuboresha huduma za tiba kwenye maeneo waliyotoka na hivyo itasaidia kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali na ngazi mbalimbali za utoaji huduma za tiba nchini.
Naye Mkuu wa huduma za Maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa amewasisitiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kufanyia tathimini ya ufanisi “Calibration” wa mashine zote kwa kuwatumia wataalam wa maabara na zile zinazotakiwa kufanywa na Shirika la Viwango (TBS) wanafanyia pia kwani ndio wenye mamlaka.Aidha, Torokaa amewataka Mameneja na Waratibu wa maabara wa Mikoa na Wilaya kuhakiki uwezo wa mashine “Method Verification” kupima na kutoa majibu yaliyo sahihi hivyo kila kipimo kithibitishwe kama kinatoa majibu ya wagonjwa yaliyo sahihi.
“Jambo la tatu tunalosisitiza ni wataalam wetu kupimwa umahiri kwa kuhakikisha mameneja na waratibu wetu wa Mikoa na wilaya wanasimamia watoa huduma wetu ambao ni wataalamu wa maabara wanafanyiwa umahiri kama wana uwezo wa kutumia hiyo mashine,kifaa na kutoa majibu ikiwemo uwezo wa tafsiri majibu ambayo yanaenda kwa Daktari kufanya maamuzi kwa mteja.
Aliongeza kuwa kila kipimo lazima kifanyike kidhibiti ubora kabla maabara haijatoa majibu kwenda kwa daktari kuhakikisha inadhibiti majibu hayo ndani ya maabara kwa kila kipimo pamoja na kuhakikisha maabara inashiriki sampuli zingine ndani na nje ya nchi ili kuweza kujipima kama wanaweza kutoa majibu yaliyo sawa.
Naye Meneja wa Maabara wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga-Bombo Sinde Mtobu amesema maabara yao imekuwa miongozi wa uboreshaji wa huduma nchini na kuwa katika ngazi ya nyota nne hivyo wanasubiri kupata ithibati ya kimataifa IS0-15-18-9 kwenye huduma za ubora kwa ujumla hivyo wapo miongoni mwa maabara 27 nchini.
Ametaja moja ya eneo ambalo wamefanya vizuri kwenye maabara ni kuwawezesha wataalam wa maabara kwenye umahiri kwa kusimamia miongozo yote pamoja na eneo la uhakiki ubora wa huduma zao kabla ya kwenda kwa daktari.