Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wafanyakazi wa Wizara yake kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa ubunifu, kujituma, watumie TEHAMA kutatua changamoto za wananchi, wahakikishe TEHAMA inachangia kikamilifu pato la taifa kwa kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni barabara ya dunia ya sasa ya kidijitali
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo mpya
Amewataka wafanyakazi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na yeye sio muumini wa michakato bali anahitaji kuona matokeo ili kuhakikisha kuwa TEHAMA inatumika kujibu changamato za wananchi ili mwananchi apate huduma za Serikali mahali popote alipo badala ya kufuata watendaji walipo
“Nataka kuona bwana shamba anatumia mawasiliano kupata mbegu, pembejeo na wakulima watumie TEHAMA kupata masoko, waalimu tulionao watumie TEHAMA kufundishia wanafunzi kwa kuwa Wizara hii ina dhamana na masuala ya TEHAMA, ndiyo yenye sera ya TEHAMA, inatoa miongozo, sheria, kanuni na viwango kwa taasisi zote za Serikali, sekta binafsi na wananchi”, amesisitiza Dkt. Ndugulile
Amefafanua kuwa sasa hivi Serikali inatumia fedha nyingi kununua mifumo ya TEHAMA nje ya nchi, hivyo anataka wabunifu wa TEHAMA wazuri waliopo nchini watumike kutengeneza mitandao yetu ya kijamii na mifumo yetu ya TEHAMA ambayo ina jibu changamoto za wananchi ili Tanzania tuwe na mitandao yetu na mifumo yetu ya TEHAMA ili kuongeza pato la Taifa
Na Prisca Ulomi, WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kikao hicho kitawawezesha wafanyakazi kuwa na dira na mwelekeo wa pamoja katika kutekeleza majukumju ya Wizara mpya na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Waziri kwa kikao hicho na kuongeza ari kwa wafanyakazi kutumikia wananchi
Naye Mwenyekiti wa TUGHE wa Wizara hiyo, Laurencia Masigo amemweleza Dkt. Ndugulile kuwa wafanyakazi wako tayari kufanya kazi kwa ushirikiano, kujituma na kushirikiana na Menejimenti na kushauri yapi yafanyike katika nyanja ya TEHAMA ili kukuza uchumi wa taifa letu