RC MAHENGE AMEAGIZA MKANDARASI KUTOLIPWA FEDHA HADI AREKEBISHE MAPUNGUFU KWENYE DARAJA ALILOJENGA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amemuelekeza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda kutomlipa mkandarasi Musons Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga wa daraja la Chinyasungwi ambao umepinda.

Dokta Mahenge ametoa maelekezo hayo Januari 5,2020 wilayani Mpwapwa akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maeneo ya barabara yaliyoathiriwa na mvua ambapo serikali imezitengea fedha na kuanza ukarabati ikiwemo ujenzi wa madaraja.

Ad

Maeneo hayo ni barabara ya Pandambili-Mlali-Mpwapwa hadi Nghambi,daraja la Chinyasungwi na eneo la Iyoma ambapo zaidi ya Sh Bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo.

“Mkandarasi huyu anatakiwa alipwe Sh Bilioni 1.109 lakini nikiangalia hapa naona kabisa ukuta mmoja wa ukingo wa daraja umepinda lakini pia upana wa ukuta huo naona ni mwembamba ilhali eneo hili linapita maji mengi,nikuelekeze Meneja usimlipe mkandarasi fedha hadi arekebishe,”aliagiza.

Sambamba na hilo amesisitiza uwepo wa usimamizi katika maeneo yote ambayo ujenzi unaendelea ili makosa kama hayo na mengine yasiweze kujirudia.

“Kama ukuta unatakiwa kujengwa kwa centimeter 30 ukipunguza hata centimeter 2 unaongelea kupunguza saruji,mchanga na ukipiga hesabu unaona kabisa fedha nyingi zinakuwa zimepotea,hivyo ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na usimamizi wa karibu wakati wote,,”alisisitiza Dkt Mahenge.

Mbali na maagizo hayo amemuagiza mkurugenzi wa Bahati Investment anayejenga barabara kipande Cha Iyoma kuongeza vitendea kazi na kufanya kazi usiku na mchana Ili mvua ikitokea isiweze kuathiri kazi inayoendelea na hivyo kupelekea barabara hiyo kutokupitika.

Awali Mkuu wa Wilaya hiyo Jabir Shekimweri ameishukuru serikali kwa kupeleka fedha na kuwezesha ujenzi katika maeneo hayo kuendelea kufanyika na hivyo kuboresha miundombinu iliyopo.

“Eneo hili la daraja la Chinyasungwi yanapita Maji mengi mengine kutoka Mkoani Manyara na katika mvua iliyonyesha mwaka jana kuna kitongoji kilikuwa kisiwa,familia 22 zilikwama huko ikabidi tutafute boti kwa ajili ya kuwatoa,hivyo uwepo wa daraja hili utasaidia Sana kupunguza changamoto hiyo,”alisema Shekimweri.

Amesisitiza suala la kuimarishwa kwa usimamizi katika maeneo yote yanayoendelea na ujenzi ili kazi inayofanyika iendane na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali.

“Kila mmoja wetu awe mzalendo,aumie kuona kazi inayotarajiwa haikamiliki na kuwa katika kiwango bora, tuimarishe usimamizi,tutunze mazingira Ili kuzuia wingi wa maji yanayokuja hapa na katika hili niombe tu kwenye vikao vyetu vile vya kata ajenda ya utunzaji wa mazingira iwe miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika vikao hivyo,”alisisitiza.

Kwa upande wake kaimu Meneja wa TANROADS mhandisi Salome Kabunda amesema mipango ya muda mfupi ni kuhakikisha wanakarabati barabara hiyo Ili iweze kupitika katika kipindi hiki ambacho wanasubiri mipango ya muda mrefu ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

“Hapa tunaendelea na ukarabati ili barabara hizi ziweze kupitika,lakini kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ilivyoahidi kujenga kwa kiwango cha lami kazi hiyo tutaitekeleza,”alisema.

Wananchi wanasema changamoto wanayoipata kwenye usafiri wakati wa mvua ni kubwa sana hivyo kuiomba serikali kuendelea kuwasaidia.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango, tarehe 01 Novemba 2024 ameungana na kuongoza Waombolezaji Katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo,jijini Dar-es-Salaam, kuaga mwili wa marehemu Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali David Bugozi Musuguri

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *