WAZIRI AWESO AMUAGIZA KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI KUTENGUA UTEUZI WA MENEJA WA RUWASA MKOA WA MARA

Waziri wa Maji, Mhe.  Jumaa Aweso (Mb) amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kutengua uteuzi wa Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick Chakka na mwenzake wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Marwa Murasa kwa kushindwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maji.

Maelekezo hayo yametolewa Wilayani Tarime  tarehe 5 Januari, 2021 alipokuwa kwenye mradi wa maji wa Magoto ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Mara.  

Ad

Awali akipokea taarifa ya miradi, Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Waziri Aweso alisisitiza kwamba taarifa haina uhalisia na aliwaelekeza wataalam hao kueleza halihalisi ya miradi na sio kudanganya.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisisitiza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Magoto Wilayani Tarime Mkoani Mara.

Akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa taarifa, Mbunge wa Tarime Vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mwita Waitara (Mb) ambaye aliambatana na Waziri Aweso alimueleza kuhusu  adha ya huduma ya maji kwa wananchi wa Tarime.

Mhe. Mwita alisema kwamba miradi mingi ya maji Wilayani Tarime inachangamoto na hivyo alimuomba Waziri Aweso kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaohusika kuchelewesha utekelezwaji wa miradi

Taarifa ya miradi sambamba na maelezo ya Naibu Waziri Mwita na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri kuhusu hali halisi ya miradi ya maji wilayani humo ilimsukuma Waziri Aweso  kutofuata ratiba ya kukagua miradi iliyokuwa imepangwa na wataalam hao na badala yake alielekeza kupelekwa kwenye miradi mingine yenye changamoto ambayo haikuwepo kwenye ratiba.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wanaonufaika na mradi wa Magoto. Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga, John Magogo.

“Nimepitia taarifa ya wataalam wetu hapa na hii ratiba waliyopanga sikubaliani nayo, sasa nataka mnipeleke kwenye miradi mingine na siyo hii mliojipangia nyinyi ili tu kunifurahisha,” Waziri Aweso aliwaelekeza wataalam hao.

Waziri Aweso aliijadili taarifa hiyo ya utekelezwaji wa miradi Wilayani Tarime na huku akimtaka Meneja huyo wa Mkoa kueleza hali ya mradi mmoja baada ya mwingine na huku akibainisha kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti ambacho kilipaswa kuwa kimetumika kutekeleza miradi.

“Bora hata kisingizio ingekua fedha kama ambavyo hua mnadanganya lakini sasa hapa Mkoani Mara tumeleta zaidi ya shilingi bilioni nane na fedha iliyopo kwenye akaunti kwa sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 3 hivi ni nani atakuelewa watu hawana maji wewe kwenye akaunti unayo fedha ya kutosha,”  Waziri Aweso alihoji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kulia) akikagua chanzo cha maji mradi wa Magoto. Kushoto ni Mbunge wa Tarime Vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara.

Alisema lengo la kuanzisha RUWASA ni kuhakikisha wananchi wanapata maji na kwamba maelekezo ya awali ni kwamba kabla utekelezwaji wa miradi haujaanza kila Meneja wa RUWASA Mkoa alipaswa kuwasilisha taarifa ya kuainisha miradi kichefuchefu yaani miradi iliyokuwa ni kero kwa wananchi lakini RUWASA Mkoa wa Mara haikufanya hivyo.

“Wananchi wanachohitaji ni maji bombani, hatutokubali kumuona Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli akiumia na kusononeka kuona wananchi wake wanateseka hawana maji na sisi tupo, hii haipendezi hata mbele za Mungu, tumemuahidi kufanya kazi na sasa tunahakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama,” alisema Waziri Aweso.

Aliongeza kuwa taarifa ya hali ya miradi wilayani humo inasikitisha kwani tathmini aliyoifanya inaonyesha miradi mingi imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 lakini haitoi maji na hivyo aliwataka wataalam kote nchini kutumia vyema utaalamu wao badala ya kujiamulia kujenga miradi kiholela.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza kwa njia ya simu na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Magoto Wanaoshuhudia ni wananchi wanaonufaika na mradi huo.

“Haiwezekani mradi upo asilimia 98 na hautoi maji, unawezaje kujenga tenki hali yakuwa huna uhakika kama maji yapo? Ulipaswa kujiridhisha na chanzo chako kwanza ili kuhakikisha maji yapo yakutosha na hatua zingine zinafuata,” Waziri Aweso alisisitiza.

Baada ya mahojiano ya muda mrefu na Mameneja hao kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Waziri Aweso alielekeza msafara alioambatana nao kutembelea mradi wa maji wa Magoto ili kujionea hali halisi ya utekelezwaji wake.

Aidha, mara baada ya kutembelea mradi huo na kujionea hali halisi sambamba na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo, Waziri Aweso alijiridhisha pasi na shaka kwamba mradi huo haujatekelezwa kama inavyopasa.

Hali hiyo kwa ujumla na taarifa iliyowasilishwa kwake hapo awali pamoja na maelezo ya viongozi na wananchi wa Kata ya Nyakonga ilipelekea Waziri Aweso kumuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutengua uteuzi wa Mameneja hao na alimtaka kufika Mkoani Mara ili kujionea hali ya miradi sambamba na kuunda kamati itakayochunguza miradi kichefuchefu yote mkoani humo.

“Namuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutengua uteuzi wa Mameneja hawa mara moja na wapewe wengine watakaomudu majukumu haya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na toshelevu,” alielekeza Waziri Aweso.

Alisema miradi mingi Mkoani Mara hairidhishi na hivyo ni muhimu Katibu Mkuu akaitupia jicho RUWASA hususan watendaji wake na kwamba wasiokuwa na uwezo waondolewe na alisisitiza kwamba ni muhimu kujiridhisha uwezo wa wataalam kabla ya kuwapanga.

Waziri Aweso vilevile alielekeza miradi yote ya maji iwe shirikishi, viongozi na wananchi wa maeneo husika wawe na uelewe wa pamoja wa kinachoendelea ili kuepuka kucheleweshwa ujenzi wake.

Waziri Aweso yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maji hususan inayotekelezwa maeneo ya vijijini.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *