Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya picha ya kuchora ya THE BIG FIVE mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji na Mwenyekiti wa SADC Mhe. Filipe Jacinto Nyusi katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja leo Jumatatu Janruari 11, 2021

RAIS NYUSI: RAIS MAGUFULI ANASHUGHULIKIA MAISHA YA WATU

Na Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato

Rais wa Msumbiji, Felipe Jacinto Nyusi amesema kuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anashughulikia maisha ya wananchi kwa kuendelea kuboresha sekta ya  huduma za afya nchini.

Ad

Rais Nyusi amesema hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato, iliyopo wilayani Chato mkoani Geita pamoja na kupanda kama kumbukumbu ya upendo na amani

“Nashukuru kwa Rais Magufuli kunipa nafasi ya kuweka jiwe la msingi kwa sababu Serikali inayoaangalia afya ya wananchi hiyo ni Serikali inayopenda wananchi, Rais Magufuli anashughulikia sana maisha ya wananchi wa watanzania kwa kuangalia nyumba bora za  kuishi, huduma za maji, chakula  na afya bora” alisema Rais Nyusi.

Alisisitiza “Kwa hiyo hii ni zawadi kwetu  kwa kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali hii kubwa, kule Msumbiji tumeanza (Program ya  presidential initiatives) ya kujenga hospitali kila wilaya hii ni zawadi kubwa kwetu ya  kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi  katika afya ya wananchi.

Tunatakiwa tujue watu wangapi na umbali kutoka hospitali moja hadi nyingine, sasa hiki tulichoona hapa ni mfano mzuri kwa sababu hii ni hospitali kubwa sana ambayo ipo  karibu na mikoa mitano na nchi jirani za Kenya na Uganda  naamini wataweza kuhudumiwa hapa”

Aidha, Rais Nyusi alisema kuwa mkoa wa Geita  ni tajiri kwa kuwa kuna kilimo cha mpunga,  madini ya dhahabu na uvuvi wa  samaki, hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kufanyakazi kwa bidii.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli alimshukuru Rais Mhe. Filipe Nyusi kwa kumtembelea Chato na kuongeza  kuwa  Msumbiji ni rafiki wa muda mrefu wa Tanzania na nchi hizo  zina makubaliano ya kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo biashara.

“Biashara kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka, hadi kufikia mwaka 2020 ilifikia shilingi bilioni 93.6, kuna makampuni ya Msumbiji yanafanya kazi hapa na baadhi ya makampuni ya Tanzania yanafanya kazi kule.” Alisema Rais Magufuli

Aliongeza  kuwa Januari 9, 1967 Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitembelea wilaya ya Chato na kufungua kiwanda cha pamba kilichojengwa kwa shilingi milioni 2 ambacho kilikuwa na uwezo wa kuchakata marobota 20,000.  Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Mwalimu Nyerere alichangisha fedha na yeye binafsi kuchangia shilingi 2,000 kwa ajili ya kujenga bandari ya Nyamirembe ili iweze  kusafirisha pamba kwenda Mwanza na Dar es salaam kwa hiyo wa Rais Nyusi amefika eneo ambalo alifika Mwalimu Nyerere

“Kwetu sisi tunaona hii ni zawadi kubwa kwa wewe kuja kuzindua hospitali hii ambayo ni kubwa na itahudumia pia nchi za jirani.Nawashukuru Wizara ya Afya na Wakandarasi, nitawabana Wizara ya Afya  ili hospitali hii ikamilike mara moja.” Alisema Rais Magufuli

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alisema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato ilikadiriwa kutumia sh. bil.16, Serikali imeshatoa sh. bil.14 ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na makabidhiano yanatarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2021.

Aliongeza kuwa awamu ya pili ya ujenzi  imeshaanza kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 14 ambapo mpaka sasa Serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 na utekelezaji wake umefikia asilimia 37.

“Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya milioni 14 ambapo kwa siku itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya 700 – 1000.” Alisema Waziri huyo wa Afya

Alifafanua kuwa maboresho ya afya nchini  yamesaidia kuharakisha matibabu bobezi na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje kutoka wagonjwa 682 mwaka 2014/15 hadi wagonjwa 42 mwaka 2020.

Rais wa Msumbiji, Felipe Jacinto Nyusi yupo nchini kwa ziara ya siku moja ambapo atafanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu namna  ya kuboresha maisha  wananchi  pamoja na usalama.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *