WAZIRI LUKUVI ATAKA WATENDAJI WA MITAA KUSIMAMIA ARDHI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanashusha usimamizi wa masuala ya ardhi kwa watendaji wa mitaa na vijiji na sio kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji kama ilivyo sasa ili kuepuka migogoro ya ardhi, ujenzi holela na kurahisisha ufuatiliaji makusanyo ya kodi ya pango la ardhi.

Akizungumza wakati akikagua ofisi ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Singida ambapo alikutana na Bibi Maria Shama na Mwanae Haruna Mkama waliokuja kufuatilia suala lao la mgogoro ardhi katika ofisi hiyo, Waziri Lukuvi alisema ni vyema wakurugenzi katika halmashauri nchini kuwapa wajibu watendaji wa mitaa na vijiji kwa barua kusimamia sheria katika masuala ya ardhi na sio kuwaachia wenyeviti wa mitaa ambao wamekuwa wakichukua jukumu hilo na kusababisha migogoro. 

Ad

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema Watendaji wa Mitaa na Vijiji watakaokasimishwa mamlaka ya usimamizi ardhi katika maeneo yao hawatakuwa na jukumu la kugawa, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi bali kuangalia yanayoendelea katika mitaa yao na wakikuta ukiukwaji wowote kama vile ujenzi holela basi watakuwa na wajibu wa kusitisha.

 ” Afisa ardhi katika wilaya hawezi kujua yale yanayoendelea kwenye mtaa au kijiji na hata suala la kodi  mkiwatumia watendaji wa mitaa wataweza kusaidia kuwabaini wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kirahisi”

Ametaka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri kuhakikisha wanatengeneza majedwali maalum yenye orodha inayoonesha kila mmiliki wa kiwanja kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa mitaa kuwajua wamiliki katika maeneo yao.

 ” Kumbukumbu zote za masuala ya ardhi wajulishwe watendaji wa mitaa na vijiji ili waweze kufuatilia katika mitaa yao maana katika suala la hati za kimila tumefanya vizur ngazi ya vijiji ila suala la Hati Miliki za Ardhi bado tuko nyuma maana tumeficha taarifa wilayani” alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alizitaka ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha zitatoa elimu kwa watendaji wa mitaa na vijiji ili kuwajengea ufahamu wa masuala ya ardhi na kuwawezesha kusimamia vyema masuala hayo katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hata kama Manispaa imepanga matumizi bora ya ardhi ni vyema matumizi yake yakawekwa kwenye vipande vya ngazi ya mitaa na kusisitiza kuwa kazi hiyo ni ya halmashauri kwa kuwa mitaa ni jicho lake la kutoa taarifa katika masuala mbalimbali yakiwemo yale ya ardhi.

Katika ziara yake Waziri wa Ardhi mbali na kutembelea halmashauri za wilaya ya Singida na Ikungi na kusisitiza kuwa halmashauri ndizo zenye jukumu la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo yake na jukumu hilo siyo la maafisa ardhi.

Lukuvi alisema Halmashauri zote zijue zina wajibu wa kusimamia ardhi katika maeneo yao na ilichofanya Wizara ya Ardhi ni kuwapatia wataalam watakaowasaidia kujua namna bora  ya kutumia ardhi vizuri.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *