KAMATI YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA WIZARA KUANZA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO YA VIFURUSHI

Na Prisca Ulomi, WMTH

Wizara Mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyoundwa tarehe 5 Desemba, 2020 imekutana kwa mara ya kwanza na kufanya kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa menejimenti na wakuu wa taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) na Tume ya Taifa ya TEHAMA (ICTC) Iimekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na kuwasilisha taarifa ya muundo na majukumu yao

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akiwasilisha taarifa ya muundo na majukumu ya Wizara na taasisi zake kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Dodoma. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew na wa tatu kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso amesema kuwa Wizara na taasisi zake imekutana na Kamati hiyo ili kutoa mwelekeo wa namna Wizara mpya itakavyojiendesha na kutekeleza majukumu yake na wameipongeza UCSAF na TCRA kwa kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kudhibiti matumizi ya huduma za mawasiliano na vifaa vya TEHAMA nchini

Kakoso amesema kuwa Kamati imeridhishwa na muundo, mipango na majukumu ya Wizara na taasisi zake na imeilekeza Wizara kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuliondolea mzigo Shirika la TPC la kulipa pensheni kwa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo tangu mwaka 2016 hadi sasa kiasi cha bilioni kumi zimetumika kulipa wastaafu hao na taasisi za Serikali zinazodaiwa na TTCL kiasi cha shilingi bilioni 22 hadi mwezi Desemba, 2020 zilipe madeni yao kutokana na kutumia huduma walizopewa na TTCL za simu na data

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso akizungumza na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kulia), Menejimenti ya Wizara hiyo na watendaji wa taasisi zake wakiwa kwenye kikao cha Kamati hiyo na Wizara kilichofanyika Dodoma. Aliyeketi wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew na wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula

Vile vile, wamempongeza Dkt. Ndugulile kwa kuanza kuchukua hatua na kushughulikia changamoto na malalamiko ya wananchi wanaotumia vifurushi na bando za simu za mkononi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi na wameitaka Wizara hiyo kushughulikia mwingiliano wa mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani ili wananchi waishio maeneo hayo waweze kupata huduma za mawasiliano

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Zainab Chaula amesema kuwa Wizara imekutana na Kamati hiyo kwa mara ya kwanza na iko tayari kushirikiana na Kamati kuongeza msukumo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula baada ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) kuwasilisha muundo na majukumu ya Wizara hiyo na taasisi zake, Dodoma

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa wataendelea kujenga minara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani, yenye milima na miinuko na watatumia teknolojia rahisi kuongeza wigo wa upatikanaji wa mawasiliano nchini

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Zuberi Kuchauka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuunda Wizara mpya kwa kuwa dunia imehamia kwenye mitandao, inajikita kwenye uchumi wa kidijitali na TEHAMA, ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa na ameitaka Wizara hiyo kuwekeza kwenye tafiti za TEHAMA, kuwaendeleza wataalamu wa TEHAMA, kutumia TEHAMA kulinda usalama wa taifa kwenye mtandao  na wameitaka Wizara kutambua kuwa Wizara hii ni kubwa na ishughulikie masuala yote yanayohusu TEHAMA nchini

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.