WAZIRI KALEMANI APONGEZWA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KWA KASI YAKE YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imempongeza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kwa kasi yake ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya vijiji vyote nchini vimepelekewa huduma ya umeme.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Seif Khamis Gulamali baada ya kuwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara ya Nishati kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika leo tarehe 20 Mwezi Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma.

Seif Khamis Gulamali amesema, kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa na yawezekana Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika inayoongoza katika usambazaji wa umeme vijijini.

Akizungumza kufuatia pongezi hizo, Waziri Kalemani amesema, Wizara ya Nishati itahakikisha vijiji vyote 2200 vilivyobakia ambavyo bado havijaunganishwa na umeme, vinapatiwa huduma hiyo ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.

Akijibu swali kuhusu maeneo yenye changamoto ya ukatikaji wa umeme hapa nchini, Waziri Kalemani ameeleza kuwa, kwa upande wa Dodoma , Dar-es-salaam na Mwanza, Wizara ya Nishati kupitia ofisi ya TANESCO imefunga mitambo yenye uwezo wa kutoa umeme wa kutosha hivyo endapo kutatokea kukatika kwa umeme  kutakuwa kumetokana na hitilafu ya kiufundi.

Dkt. Kalemani ameeleza bayana kuwa, kwa upande wa jiji la Dodoma, Wizara ya Nishati kupitia Shirika lake la TANESCO imekamilisha Mradi wa MW 400 na mahitaji ya Dodoma kwa sasa ni MW 45 tu hivyo umeme upo wa kutosha. “Iwapo kutatokea kukatika kwa umeme kwa jiji la Dodoma hiyo itakuwa kuna tatizo la kiufundi lakini si kwa mitambo ya umeme kuelemewa .” Amesema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani amekiri kuwa, kulikuwa na tatizo la umeme kwa mkoa wa Ruvuma isipokuwa eneo la Masasi na Tunduru na kueleza kuwa kuna vifaa vya kuboresha nguvu ya umeme ( Automatic Voltage Regulators – AVR ) vinaendelea kufungwa ili kuongeza umeme uwe mkubwa kwa ajili ya watumiaji.

Dkt. Kalemani amemhakikishia Mhe. Mha. Stella Manyanya mbunge wa Nyasa aliyehoji kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme katika jimbo la Nyasa kuwa, ufungaji wa vifaa vya AVR utakuwa umekamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa na hivyo upatikanaji wa  umeme katika maeneo husika utaimarika.

Akijibu swali kuhusu ratiba ya utekelezaji wa kazi za Wakandarasi katika maeneo yanayopitiwa na miradi ya umeme, Waziri Kalemani amesema, “tumewasihi sana Wakandarasi wanapofika kwenye maeneo husika, wakutane nanyi Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Wilaya. kwanza, kutoa taarifa kuwa wameingia kwenye maeneo yenu lakini pia wajue wanaanzia maeneo gani yenye kero ili kushauriana nao mahali pa kuanzia. Tutakapokuwa tunazindua tutawakabidhi kwenu Wakandarasi hao ili mkae nao wajue waanzie wapi.” Amesema Dkt. Kalemani.

Makamu M/Kiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Seif Khamis Gulamali na Katibu wa kamati hiyo Bi. Felister Mgonja pamoja na wajumbe wa Kamati tajwa hapo juu, wakifuatilia kwa makini maelezo ya Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati Kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo tarehe 20 Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri Kalemani, ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Leonard Masanja.

Akielezea kuhusu tatizo la upatikanaji wa mafuta kwa maeneo ya vijijini na miji midogo, Dkt. Kalemani ameieleza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, Wizara ya Nishati ina mpango wa kuendelea kusambaza Vituo vya Mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa Nishati ya Mafuta na usalama kwa watumiaji wa maeneo tajwa yanayokabiliwa na upungufu wa mafuta.

Ad

Waziri Kalemani amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa suala hilo, kanuni zinapitiwa ili kupunguza gharama za uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo ikizingatiwa kuwa kujenga kituo cha kawaida cha mafuta inagharimu shilingi 500,000,000/= ambazo ni nyingi kwa wawekezaji wa vijijini.

Dkt. Kalemani amesema. Wizara ya Nishati, inafikiria kujenga vituo rahisi vya pampu moja, ambavyo uwekezaji wake utakuwa nafuu.

Kikao hicho cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichoanza leo jijini Dodoma kimekutana na Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake na kitarajiwa kukamilika tarehe 22 Januari, 2021. 

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA SULUHU AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WAZIRI WA NCHI, WIZARA YA MAMBO YA NJE YA SHIRIKISHO LA JAMHURI YA UJERUMANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akizungumza na kuagana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.