Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema serikali inaweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa mazao ya mafuta ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta inayotokea nchini na kupunguza kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Akizungumza leo mara baada ya kutembelea kiwanda cha mafuta ya alizeti cha PYXUS kilichopo Kizota jijini Dodoma,Profesa Mkenda amesema ni wakati sasa wa wakulima kuandaa mashamba na kutumia mbegu bora na watalaam.
“Sisi kama serikali tunajipangak uhakikisha kunakuwa na mbegu za kutosha,tunaweka nguvu kubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya mafuta,ukiangalia sasa hivi tunatumia takribani nusu trilioni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje,sisi kwenye mfumo rasmi tunazalisha asilimia 47 tu,lakini wakulimawetu wanahitaji fedha,”alisema.
Alitoa wito kwa wakulima kujitokeza kwa wingi kuandaa mashamba na kutumia wataalam katika kilimo hicho.
Aidha aliwataka wakulima kutumia fursa ya uhaba wa mafuta iliyopo kwa kuongeza uzalishaji wa alizeti na mazao mengine ya mafuta nchini na kutumia changamoto hiyo kama fursa ya kujiongezea kipato,kuongezea nchi kujitegemea kwenye mafuta ya kula na kupata fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa hizo nje ya nchi.
Profesa Mkenda amekemea suala la urasimu lililopo bandarini katika utoaji wa vibali vya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na kusema yoyote mwenye tabia hiyo atafute shughuli nyingine ya kufanya.
“Utaratibu mbovu huu,haiwezekani tukakwamisha na mtu mmoja wakati tunahitaji wawekezaji,kuna makontena yapo bandarini kuna maafisa wamekalia tu hawataki kutoa vibali,natoa wito kwa maafisa hao wajue kwenye uchumi tunaoenda lazima twende kwa kasi,sisi hatujakataza kuuza mafuta ghafi nje,nitaongea na wizara ya viwanda na biashara kuhakikisha afisa anayechelewesha apangiwe majukumu mengine au akalime alizeti,”alisisitiza.
Alisema serikali itawaunga mkono wawekezeji hasa wa sekta binafsi,tutawatetea na kuwalinda ili kufikisha lengo tulilojiwekea la kujitegemea katika mafuta ya kula.
Meneja wa wakulima wadogo wa Pyxus Edwin Shio alitaja changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo wakulima kukiuka masharti yaliyopo kwenye mkataba na kupata kibali cha kusafirisha mafuta ghafi kwenda nje ya nchi.
“Tunahitaji kupeleka mafuta nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni ili kuendeleza uzalishaji wa kiwanda chetu lakini changamoto kubwa tunayoipata utakuta mzigo unakaa bandarini zaidi ya wiki hadi mwezi hivyo inakuwa kikwazo kwetu,tunaomba serikali itusaidie ili tupate export ya mafuta tunayotarajia kupeleka nchini Switzerland,”alisema.