TANESCO DODOMA YAPEWA MIEZI 6, MAKAO MAKUU YA NCHI KUPATA UMEME YOTE

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Dodoma kuwa, ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa, Vijiji na maeneo yote ya mkoa huo yawe yamepata umeme, kuunganisha na kuwawashia wateja, atakayeshindwa kutekeleza hilo atakuwa amejifukuza kazi mwenyewe.

Dkt. Kalemani alisema hayo, wakati wa mkutano wake na wafanyakazi wa TANESCO wa Mkoa wa Dodoma, wenye lengo la kufahamiana, kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi hao pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.

Aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa, wao ndiyo wenye dhamana na jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Mkoa wa Dodoma unapata umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo yote, kuunganisha na kuwawashia wateja.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoa wa Dodoma, (hawapo pichani) wakati wa mkutano wake na wafanyakazi hao uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.

Dkt. Kalemani alisisitiza kuwa, mkoa huo kwa sasa una wakazi wengi sana na bado wanaendelea kuongezeka kwa kuwa ni Makao Makuu ya Nchi, umeme mwingi unahitajika katika shughuli mbalimbali, hivyo lazima kila mfanyakazi awe sehemu ya shirika hilo na afanye kazi kwa kasi zaidi, ubunifu mkubwa na kwa usahihi ili kukidhi mahitaji ya umeme na kuboresha zaidi huduma zitolewazo na shirika hilo.

“Sitakubali kupata aibu ya baadhi ya maeneo na Vijiji vya Makao Makuu ya Nchi, kutokuwa na umeme, mkoa huu unazaidi ya Megawati 400 za umeme, lakini matumizi ni Megawati 45 tu kwa sasa, wakati kuna wateja wengi ambao wanahitaji umeme na maeneo mengine bado hayajafikiwa kabisa na huduma hiyo,TANESCO  Dodoma fanyeni kazi!”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Hata hivyo alitoa siku 14, kwa shirika hilo mkoani humo kumfikishia taarifa ya namna walivyojipanga katika kusambaza umeme kwa wananchi, kuunganisha wateja wa zamani na kupata wapya, kuzalisha na kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Meza kuu wakiwa wameshikana mikono kuimba wimbo wa wafanyakazi unaosema Mshikamao Daima, wakati wa mkutano Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na wafanyakazi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoa wa Dodoma. uliofanyika Januari 22, 2021 mkoani humo.

Vile vile alipiga marufuku kwa baadhi ya watumishi wenye tabia ya kuchelewesha majalada ya kazi, kwa kusema kuwa vitendo hivyo vinachelewesha utendaji kazi na kutotimiza malengo kwa wakati.

Alisisitiza kuwa, asilimia kubwa ya utendaji kazi katika ofisi hufanyika kwa mfumo wa maandishi kupitia majalada, endapo mmoja atachelewa au kukwamisha, kazi husika itachelewa na kutotekelezeka kwa muda uliopangwa.

“Ni mwiko na marufuku kukaa na jalada mezani zaidi ya siku moja ofisini, kama huwezi kulifanyia kazi sema au upeleka kwa wanaoweza kulifanyia kazi, tunataka kazi ziende haraka na kwa wakati, ukiona huwezi kufanya kazi kwa kasi hii ninayotaka ni bora uondoke ofisini! Alisema Dkt.Kalemani.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Wizara ya Nishati, Daniel Machunda (kushoto) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent luoga, (kulia) wakibadilishana mawazo, wakati wa mkutano Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoa wa Dodoma uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani  aliiagiza TANESCO, kuangalia upya utaratibu wa kuajiri au kuwapa kazi wafanyakazi wa muda maalum( STE) ambao muda mwingi wanakuwepo maeneo kazi (Site) kufanya kazi za kuchimba mashimo, kusimika nguzo na kuvuta nyaya.

Aidha alitaka STE wasiokuwa na mikataba wapewe mikataba, wenye sifa ya ajira waajiriwe na wale wasiokuwa na sifa na wamefanya kazi muda mrefu, wapewe mafunzo maalum ili wapate ajira.

Pia alitaka shirika hilo kuboresha maslahi wa wafanyakazi hao na kuangalia namna bora ya kuwapa motisha sehemu za kazi waweze kufanya kazi zao kwa furaha, amani na utulivu na kuboresha utendaji kazi wao.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Adam Zuberi, (kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Daniel Machunda (katikati) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent luoga, (kulia) wakisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ( hayupo pichani), wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na wafanyakazi shirika hilo wa Mkoa wa Dodoma uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.

Sambasamba hilo, alitoa miezi miwili kwa wapimaji na watathmini ( Surveyor) pamoja na watoa namba (Control Number) kwa wateja kwa ajili ya kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, kubadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na taaluma zao, na atakayeshindwa kufanya hivyo afukuzwe kazi.

Dkt. Kalemani aliweka wazi kuwa watumishi wa vitengo hivyo wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutotekeleza majukumu yao kwa wakati na kuchelewa kutoa huduma kwa wateja.

Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Dodoma wakishikana mikono kuimba wimbo wa wafanyakazi unaosema Mshikamao Daima, wakati wa mkutano Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na wafanyakazi hao uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.

 Na Zuena Msuya, Dodoma

Aidha aliliagiza shirika hilo kuwapatia pikipiki wafanyakazi wote wa kitengo tathmini na upimaji kurahisisha utendaji kazi wao.

Akizungumzia kitengo cha huduma kwa wateja, Dkt. Kalemani alitaka wahusika kutumia lugha rafiki na zinazofaa kwa wateja, kuweka watoa huduma vijana ili waweze kufanya kazi kwa kasi na haraka zaidi.

“Vitengo hivi vinalalamikiwa sana, wanatakiwa kubadilika, unakuta mteja amejipanga na yupo tayari kupata huduma, lakini mtathimi hafanyi kazi yake, halikadhalika na mtoa namba, ukija huduma kwa wateja anatumia lugha ya mbaya, jamani badilikeni la sivyo mtajifukuza kazi wenyewe”, alisema Dkt. Kalemani.

Akizungumia zoezi la kuwaunganishia umeme wateja, Dkt. Kalemani alisema wateja wote wanaohitaji umeme waunganishiwe kwa gharama halisi zilizoelekezwa na Serikali, marufuku kwa mteja kulipa zaidi ili apate huduma hiyo kwa haraka na mapema zaidi ya wenzake, kufanya hivyo ni kutoa Rushwa.

Alisema kuwa kuanzia mwezi Februari serikali itaanza kusambaza na kuunganisha umeme kw vijiji vyote nchini vilivyosalia na kazi hiyo itafanyika kwa kipindi cha miezi 18.

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.