????????????????????????????????????

NAIBU WAZIRI SILINDE AAGIZA TSC IPEWE OFISI ZENYE HADHI

Na Veronica Simba – TSC

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde amewaagiza Wakurugenzi wa Wilaya kote nchini, kuhakikisha wanawapatia ofisi zenye hadhi, watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika maeneo yao.

Ad

Ametoa maagizo hayo leo, Januari 25, 2021 mjini Morogoro wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume.

Naibu Waziri ametoa maagizo hayo baada ya kuelezwa changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume husika, ambapo mojawapo ni ya ukosefu wa ofisi zenye hadhi kwa watumishi wa TSC hususani zilizoko katika baadhi ya Wilaya nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde (wa tatu – kulia), akiungana na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuimba wimbo maarufu wa ‘Solidarity Forever’. Naibu Waziri alifungua Mkutano huo mjini Morogoro, Januari 25, 2021. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba na kulia kwake ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

“Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanawapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume, ofisi ambazo zinaendana na hadhi ya utumishi wa umma.”

Aidha, ameitaka Tume kuhakikisha inawawezesha Walimu kujitambua na kuelewa sheria, kanuni, taratibu, haki na wajibu wao.

Vilevile, ameipongeza Tume kwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa moyo wa uzalendo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili. Pamoja na kutoa pongezi, ameitaka Tume kuendelea kutoa huduma bora kwa Walimu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), muda mfupi baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakzi wa Tume hiyo Januari 25, 2021 mjini Morogoro. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba na kushoto kwake ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

“Sote tunafahamu kuwa tunapotoa huduma bora kwa Mwalimu inamwezesha kutekeleza majukumu yake shuleni kwa ufanisi hatimaye kuinua kiwango cha elimu nchini.”

Naibu Waziri ameihakikishia Tume kuwa ushirikiano uliopo katika utendaji kazi kati ya Tume na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni endelevu. Aidha, ameongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kusisitiza kila Wilaya kuhakikisha kazi za kushughulikia masuala ya kiutumishi ya Walimu zinatekelezwa kwa ushirikiano ili kuleta tija na ufanisi katika suala zima la kuwahudumia walimu.

Awali, akiwasilisha hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Tume, Profesa Willy Komba alibainisha changamoto kadhaa zinazoikabili, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na jengo la Ofisi za Tume Makao Makuu na Wilaya.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Willy Komba (kulia), akitoa hotuba ya ukaribisho wa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde (katikati), wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo, Januari 25, 2021 mjini Morogoro. Kushoto ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya waajiri kutokuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kushughulikia masuala ya kinidhamu ya Walimu.

“Mfano kuchelewa kuwasilisha mashtaka kwa Mamlaka ya Nidhamu, kuchukua jukumu la kutoa adhabu kinyume cha utaratibu na kuwaondoa Walimu kwenye mfumo wa malipo kabla ya mchakato wa mashauri kuanza na kukamilika,” amefafanua Profesa Komba.

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa pia na Kaimu Katibu wa Tume, Moses Chitama, Menejimenti ya Tume pamoja na wawakilishi mbalimbali kutoka wilaya zote nchini.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali, Tanzania Bara. Naibu Waziri David Silinde ndiye amepewa wajibu wa kusimamia Taasisi hii pamoja na nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *