WAZIRI BASHUNGWA: SEKTA ZA WIZARA YA HABARI NI MIHIMILI MUHIMU NCHINI

Na Shamimu Nyaki – WHUSM 

Sekta za Wizara ya Habari ni sekta muhimu  zenye  mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi na kuleta  maendeleo.

 Hayo yamesemwa  leo Jijini Dodoma na Waziri  wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha Muundo pamoja na Majukumu ya Wizara hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki akipitia nyaraka za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zilizowasilishwa kwa kamati hiyo na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa (Hayupo katika Picha), January 25, 2021 jijini Dodoma . Kushoto ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale

Mhe. Bashungwa amesema kwamba Sekta ya Sanaa na Michezo zimechangia katika Ongezeko la pato la Taifa ambapo kwa mwaka 2018, shughuli za burudani zimechangia pato la Taifa kwa asilimia 13.7 na kushika nafasi ya kwanza  na  mwaka 2019 shughuli hizo zilichangia asilimia 11.2 na kushika nafasi ya tatu.

“Tunashukuru Kamati kwa kutupa mawazo chanya ambayo yatasaidia kuboresha na kuendeleza sekta hizi, naahidi mimi pamoja na timu yangu tutayafanyia kazi mawazo mliyotupa na tayari tumeanza kufanya hivyo katika sekta zote” alisema Mhe. Bashungwa.

Baadhi ya wabunge ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakitoa maoni baada ya kupokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka kwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa January 25, 2021 jijini Dodoma.

Akiendelea kuzungumza Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa Wizara tayari imeanza kutengeneza Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo pamoja na ujenzi wa Ukumbi wa Michezo na Sanaa (Sports and Arts Arena) ambayo itaanza kujengwa Jijini Dodoma.

Aidha, Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa TCRA pamoja na TRA wameanza kushirikiana namna ya  kukusanya mapato ya kazi za Sanaa kupitia njia za Kidijiti (Digital Taxation).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stasilaus Nyongo Mbunge wa  Jimbo la Maswa Mashariki ameipongeza Wizara hiyo kwa Mikakati mizuri ya kusaidia Sekta inazozisimia, huku akishauri Wizara hiyo kuongeza ubunifu katika kukusanya mapato ya Serikali kupitia Sanaa na Michezo.   

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akiwasilisha Muundo na Majukumu ya Wizara hiyo kwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii January 25, 2021 jijini Dodoma.

“Nashauri Wizara hii, Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI  kuwa na utaratibu unaotambulika wa kuendesha na kusimamia shughuli za michezo shuleni” Mhe. Nyongo.

Naye Mhe. Jumanne  Sagini Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo amepongeza juhudi za Wizara hiyo katika kutekeleza majukumu yake ambapo ameeleza kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya Sera zote zilizochini ya Wizara hiyo ili kama kuna ambazo zinahitaji marekebisho zifanyiwe maboresho ili kuendana na mahitaji ya wakati huu.

Kamati hiyo imepokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo kesho Januari 26, 2021 itapokea Taarifa ya Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.